Zoezi la kuchukua fomu za kuwania ubunge CCM limekamilika
4 Julai 2025Ni patashika majimboni. La mgambo likilia basi ujue kuna jambo. Chama cha Mapinduzi kimetaja idadi ya makada wake waliotia nia kugombea ubunge majimboni upande wa Zanzibar na Tanzania Bara, kuwa ni 4109.
Akizungumza jana, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla amesema, wingi wa uchukuaji fomu unaonyesha ni kwa namna gani chama hicho kinapendwa na watanzania.
Joto la Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani limeanza kupanda nchini Tanzania
“Chama cha Mapinduzi tumefurahishwa na hamasa kubwa iliyojitokeza na chama cha mapinduzi, nyinyi ni mashahidi uchukuaji wa fomu umevunja rekodi mwaka huu,” alisema Makalla.
Mchanganuo wa uchukuaji wa fomu ndani ya chama hicho, unaonyesha kuwa, waliochukua fomu katika majimbo 272 ya Tanzania Bara ni 3585 na 524 upande wa Zanzibar na kufanya jumla ya watia nia kuwa 4109.
Wakati hatua hii ya kwanza ikikamilika, mtanange bado unatarajiwa kwani chama hicho sasa kinakwenda kufanya mchujo wa kupiga kura za maoni kuwapata wanaokwenda kukiwakilisha chama katika majimbo.
Mchakato huu wa uchukuaji wa fomu za majimboni, umekiwezesha CCM kuvuna kiasi cha Shilingi bilioni 2.7 zilizotokana na ada za uchukuaji wa fomu, ambao ulikuwa shilingi 500,000 kwa ubunge na Tsh 50,000 kwa nafasi ya udiwani. Licha ya gharama za fomu, bado maelfu ya wana CCM walichukua fomu. Je ni maslahi binafsi au maslahi ya marefu mapana ya taifa. Nimezungumza na Mhadhiri wa Shule ya Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Sabato Nyamsenga.
“Watu wanapokwenda kwenye siasa wanaenda kwa maslahi ya umma, kwa bahati mbaya mfumo wa siasa katika nchi zetu, unakwenda katika mfumo wa gulio,” alisema Nyamsenga.
CCM yaonya hakuna anayeweza kuzuia uchaguzi mkuu
Makalla amesema kwa upande wa uwakilishi Zanzibar waliochukua fomu ni wanachama 503 na UWT ni 623 Bara na ndani yake yako 91 makundi maalum na Zanzibar wamechukua wanane na viti maalum uwakilishi ni tisa, ambapo jumla yao ni 640. Kwa upande wa Tanzania Bara Idadi ya wanawake majimboni waliochukua fomu ni 263.
Hata hivyo, kipyenga hiki ni mwanzo tu wa kipyenga kingine cha mchujo wa uteuzi wa majina matatu ya madiwani, na matatu ya wabunge ambayo yatapelekwa kamati kuu ya CCM ambayo itateua majina ya wabunge na wawakilishi kabla ya kupigiwa kura na wajumbe.