Ziara ya waziri wa nje wa Ujerumani Steinmeier mjini Washington
30 Novemba 2005Waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani ,Frank- Walter Steinmeier,amejitokeza vyema katika ziara yake ya kwanza nchini Marekani:
Ziara yake iligubikwa na taarifa kuwa shirika la ujasusi la Marekani (CIA) likisafirisha wafungwa kupitia viwanja vya ndege vya Ulaya (pamoja na Ujerumani) na juu ya kisa cha kutekwanyara kwa mjerumani nchini Irak.Hatahivyo, yabainika kwa maoni ya muandishi wetu aliopo Washington, Daniel Scheschkewitz,usuhuba kati ya Washington na Berlin, ni imara na unamudu kuhimili vishindo kama hivyo.
Kusema kweli, ziara ya kwanza ya waziri wa nje wa Ujerumani Steinmeier mjini Washington haikuanza kwa nyota njema.Habari za kutekwanyara nchini Irak kwa mtaalamu wa mambo ya kale wa kijerumani,kulimlazimisha kubakia siku nzima katika mawasiliano ya simu na kikosi maalumu katika wizara ya nje mjini Berlin.Isitoshe, Ujerumani ikihitajia sasa msaada wa Marekani nchini Irak katika kipindi ambacho wamarekani wenyewe wanaanza kuipa mgongo serikali yao kwa hali ilivyo nchini humo.
Kama msumari wa moto juu ya donda, zikachomoza taarifa kwamba shirika la ujasusi la Marekani likiwasafirisha wafungwa kupitia viwanja vya ndege vya Ulaya pamoja pia na vile vya Ujerumani.Hii ni hali ya kutatanisha iliogubika ziara ya Bw.Steinmeier.hatahivyo, Bw.Steinmeier alifaulu kumtuliza shetani kwa mbinu zake za kidiplomasia na za ujuzi wa kazi yake.
Marekani nayo ikajitolea haraka kuisaidia Ujerumani katika kumkomboa habusu wa kijerumani nchini Irak.Kwani, maarifa na ujuzi wa marekani pamoja na mawasiliano yake ilionayo ,yote hayao yaweza kuchangia kuokoa maisha ya mateka huyo.
Zaidi ya kisa cha utekajinyara, imebainisha jinsi gani mada ya kusafirishwa kisirisiri kwa wafungwa ,hakukuweza kuharibu tena uhusiano kati ya Ujerumani na Marekani.
Bw.Steinmeier, alizusha swali hilo wakati wa mazungumzo yake na waziri wa nje wa Marekani Dr.Condoleeza Rice nae akamhakikishia pamoja na nchi nyengine za Ulaya kuwa mkasa huu utafafanuliwa haraka.Ufafanuzi huo utafanyika namna gani,itabidi kusubiri na kuona.
Si muda mrefu nyuma ,ilikua tabia ya Marekani kupinga kujiingiza kokote kule kwa ujerumani katika maswali kama hayo.Hivi sasa lakini,Marekani inatia maanani wasi wasi wa nchi za Ulaya juu ya mada kama kukiukwa kwa haki za binadamu na mikataba ya kimataifa.
Nia njema iliooneshwa na pande zote mbili hatahivyo, haikuzuka bila ya sababu.Mbinyo unaozidi wa wananchi wa marekani kutaka majeshi ya Marekani yaondoke Irak haraka iwezekanavyo ,kunaulazimisha utawala wa George Bush,kusaka ushirikiano na nchi nyengine-kinyume na hapo kabla.Kwani, bila ya ushirikiano wa shirika la ulinzi la NATO,Marekani haitaweza kupunguza barabara majeshi yake nchini Irak.Hatahivyo, hii haitailazimisha Ujerumani kubadili msimamo wake wa kupeleka majeshi yake nchini Irak.Msaada katika kulifunza jeshi la Irak pia ni mchango muhimu kwavile, mwishoe, jeshi hilo litapaswa kujitwika jukumu la kuilinda Irak.
Hali ni sawa na hiyo katika mazungumzo na Iran .Ni kwa msaada wa nchi za Ulaya na wa Urusi ndio itafanikiwa kuishawishi Iran kuachana na mradi wake wa nguvu za nuklia.
Mafanikio ya juhudi za kidiplomasia zilizofanywa hadi sasa upande huo hayapo,lakini bila ya mbinyo wa pamoja kati ya nchi za Ulaya na Marekani, Teheran kamwe haitaregeza kamba.
Iwapo waziri mpya wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier katika uhusiano kati ya pande mbili za bahari ya Atlantik-Ulaya na Marekani ataseleleza mkondo ule ule mkali wa mkubwa wake Gehard Schröder au atafuata mkondo wa kuibembeleza Marekani wa kanzela mpya Bibi Angela Merkel, ni swali la kuulizwa.
Kwa hali ilivyo sasa ulimwenguni, inazilazimisha pande zote mbili kushirikiana.Katika hali kama hiyo kuwa majadiliano ya kinaganaga lakini pia kirafiki yaweza kusaidia kuliko kuendeleza uhasama,waziri mpya wa mambo ya nje Frank-Walter Steinmeier, amebainisha tena dhahiri-shahiri katika ziara yake hii ya kwanza mjini Washington.