Zelenskyy: Ukraine haitoachia ardhi yake kwa Urusi
9 Agosti 2025Mkutano kati ya Trump na Putin umepangwa kufanyika huko Alaska mnamo Ijumaa inayokuja na unazingatiwa kuwa hatua muhimu kuelekea kuumaliza mzozo wa Urusi na Ukraine.
Hapo kabla, Trump alisema yuko tayari kukutana na Putin hata kabla ya kiongozi huyo wa Urusi kukutana kwanza na mwenzake wa Ukraine.
Msimamo huo wa Trump ulizusha wasiwasi kwamba yumkini Ukraine imepigwa kumbo kwenye juhudi za kumaliza mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Katika ujumbe wake aloutuma kupitia mtandao wa Telegram, Zelenskyy amesema kuwa hadhi ya mipaka ya Ukraine, iliyoelezwa ndani ya katiba ya nchi hiyo, haiwezi kuwekwa mezani kwa majadiliano na kusisitiza kuwa amani ya kudumu ni sharti ijumuishe sauti ya Ukraine mbele ya meza ya mazungumzo.
Zelenskyy amesema Ukraine kamwe "haitoizawadia Urusi chochote kwa matendo yake" na "Raia wa Ukraine hawataisalimisha ardhi yao kwa mvamizi."
Akigusia hamkani nchini Ukraine kwamba mkutano wa Putin na Trump utayapuuza maslahi ya nchi yake na yale ya Ulaya, Zelenskyy amesema: "Suluhisho lolote ambalo halitaijumuisha Ukraine itakuwa sawa sawa na suluhisho la kupinga amani."
Maafisa wa Ukraine wameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba utawala mjini Kyiv hautakubali mkataba wowote wa amani utakaoondoa uwezekano kwa Ukraine kurejesha maeneo yake ya ardhi iliyoyapoteza kijeshi.
Mkutano wa Trump na Putin na matarajio ya ulimwengu
Trump alisema siku ya Ijumaa atakutana na Putin kujadili namna ya kumaliza vita ndani ya Ukraine.
Mkutano huo utafanyika kwenye jimbo la Marekani la Alaska na ikulu ya Urusi, Kremlin imethibitisha kuwa Putin na Trump watakutana huko Ijumaa ya Agosti 15.
Mkutano huo unaweza kuwa muhimu kwa hatma ya vita vya Ukraine vilivyoanza zaidi ya miaka mitatu iliyopita pale Urusi ilipotuma vikosi vyake vya kijeshi kwa jirani yake huyo.
Makumi kwa maelfu ya raia na wanajeshi wa pande zote mbili wameuawa. Si rahisi kusema iwapo mkutano wa Trump na Putin utamaliza mashambulizi kati ya Urusi na Ukraine kutokana na tofauti kubwa ya misimamo na matakwa ya kila upande.
Kwenye matamshi yake mbele ya waandishi habari katika Ikulu ya White House kabla ya kuthibitisha mkutano wake na Putin, Trump aliashiria kwamba mkataba wowote huenda utajumuisha "ubadilishanaji maeneo ya ardhi," kati ya Urusi na Ukraine.
Wachambuzi, ikiwemo baadhi walio karibu na ikulu ya Kremlin, wameashiria kwamba Urusi inaweza kuyaachia maeneo inayoyadhibiti nje ya majimbo manne ya Ukraine inayodai imeyanyakua.