Zelenskyy ataka shinikizo dhidi ya Urusi
24 Machi 2025Akizungumza kabla ya mazungumzo kuhusu usitishaji mapigano nchini Saudi Arabia kati ya wajumbe wa Marekani na Ukraine, Zelenskyy amesema ni lazima vikwazo dhidi ya Urusi viimarishwe ili kuzuia mashambulizi zaidi, na kuongeza kuwa wiki hii pekee silaha zaidi ya 2,600 zilitumiwa dhidi ya Ukraine, nyingi zikiwa na vipuri kutoka nje.
Soma pia: Trump na Zelensky wafanya mazungumzo kwa simu
Hata hivyo, Urusi imesema mazungumzo hayo yatakuwa magumu na kwamba ndiyo kwanza yanaanza, huku suala kuu likiwa makubaliano ya awali kuhusu kusafirisha nafaka kupitia Bahari Nyeusi.
Marekani imesema ina matumaini ya mafanikio kuhusu usitishaji mapigano katika eneo hilo, ingawa awali Rais Putin alikataa pendekezo la kusimamisha vita kabisa kwa siku 30, akipendekeza badala yake kusitisha mashambulizi kwenye vituo vya nishati pekee.