Ukraine kujiondoa kwenye mkataba wa Ottawa
30 Juni 2025Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy aidha alitia saini amri inayoanzisha mchakato wa kuiondoa nchi yake kwenye Mkataba wa Ottawa wa kupambana na mabomu ya ardhini, kulingana na waraka uliochapishwa kwenye tovuti ya rais.
"Kwa hili natoa amri ... kutekeleza uamuzi wa Baraza la Usalama na Ulinzi la Kitaifa la Ukraine la tarehe 29 Juni 2025 kuhusu kujiondoa kwa Ukraine" kwenye mkataba wa Ottawa, Zelenskyy alisema.
Uamuzi wa kuachana na mkataba huo lazima uidhinishwe na bunge la Ukraine na uwasilishwe Umoja wa Mataifa kabla ya kuanza kutekelezwa. Hatua hiyo ya Ukraine inalingana na zile zilizochukuliwa hivi karibuni na mataifa ya Baltic na Poland.
Mkataba wa Ottawa wa 1997 unapiga marufuku matumizi, uzalishaji, uhifadhi na uhamishaji wa mabomu ya ardhini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwalinda raia dhidi ya vilipuzi ambavyo vinaweza kuwalemaza au kuwaua, muda mrefu baada ya mapigano kumalizika.
Katika miezi ya hivi karibuni, Urusi imezidisha operesheni zake za kukera nchini Ukraine na kuteka maeneo zaidi.
Zelenskyy atoa wito wa vikwazo zaidi Urusi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi. Anatoa woto huu baada ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kushindwa kuafikiana kuhusu awamu ya 18 ya hatua za adhabu dhidi ya Moscow wiki iliyopita.
"Vikwazo sasa vinapaswa kuwa moja ya vipaumbele muhimu zaidi," Zelenskyy alisema katika hotuba yake ya kila usiku ya video siku ya Jumapili.
Aliongeza kuwa vikwazo vya kimataifa ni kitu "ambacho kwa uhakika kinaweka mipaka ya fursa za maendeleo ya kimkakati ya Urusi, uwezo wake, na kila siku vinatakiwa kupunguza uwezo wa Urusi kuendeleza vita hivi, vita dhidi ya uhuru wetu."
Mkuu wa ujasusi wa Urusi asema alizungumza na mkurugenzi wa CIA wa Marekani
Sergei Naryshkin, mkurugenzi wa Huduma ya Kijasusi ya Kigeni ya Urusi (SVR), alisema amezungumza na John Ratcliffe, mkurugenzi wa Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA).
"Nilipigiwa simu na mwenzangu wa Marekani, na kwa pamoja tulijiwekea uwezekano wa kupigiana simu wakati wowote na kujadili masuala yenye maslahi kwetu," Naryshkin alimwambia mwandishi wa televisheni ya serikali ya Kremlin, Pavel Zarubin.
Naryshkin hakutoa maelezo zaidi juu ya mazungumzo hayo ya simu na Ratcliffe.
CIA na SVR, ambayo mrithi wa KGB, kwa muda mrefu wamekuwa ni mahasimu wakubwa. Na kila taasisi ilianzisha kampeni za umma za kuajiri mawakala kufuatia uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine mnamo 2022.
Kulingana na vyombo vya habari vya Urusi, mazungumzo ya mwisho ya simu ya Naryshkin na mkurugenzi wa CIA ambayo yaliwekwa wazi yalifanyika mnamo Machi 2025.