Zelensky yuko Vilnius kushiriki mkutano wa NATO
2 Juni 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amewasili Vilnius ambako atashiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa washirika wa Jumuiya ya kujihami ya Nato kanda ya Mashariki na Nordic.
Zelensky anatarajiwa kufanya mazungumzo kandoni mwa mkutano huo na viongozi wa mataifa kadhaa kwa mujibu wa msemaji wake. Mkutano huo wa Vilnius unafanyika kabla ya mkutano kamili wa kilele wa jumuiya ya NATO uliopangwa kufanyika baadae mwezi huu wa Juni mjini The Hague, Uholanzi.
Zelensky ambaye anataka nchi yake ihakikishiwe usalama na jumuiya hiyo,ametaka kualikwa kwenye mkutano wa The Hague akisema ikiwa atawekwa pembeni,utakuwa ni ushindi kwa rais Vladmi9r Putin wa Urusi.
Mkutano wa leo unawashirikisha viongozi kutoka nchi za Ulaya Mashariki na Kati na wanachama wa Nato kanda ya Nordic pamoja na Zelensky na katibu mkuu wa NATO Mark Rutte.