Zelensky yuko Ujerumani kujadili na Merz vita vya Ukraine
28 Mei 2025Msemaji wa serikali ya Ujerumani Stefan Kornelius amesema mazungumzo ya viongozi hao wawili yataangazia msaada wa Ujerumani kwa Ukraine na juhudi za kupatikana makubaliano ya kusitisha mapigano na Urusi, kwa lengo la kumaliza vita hivyo vilivyodumu kwa miaka mitatu sasa.
Zelensky aliwasili mjini Berlin mapema leo asubuhi na mchana huu amekaribishwa kwa heshima ya gwaride la kijeshi katika ofisi za Kansela Merzkabla ya mazungumzo kati ya viongozi hao wawili kuanza. Aidha wanatarajiwa kujadili juhudi za Umoja wa Ulaya za kuiwekea vikwazo zaidi Moscow huku kukiwa na ukosefu wa maendeleo hadi sasa kuelekea kusitisha mapigano na hatimaye mazungumzo ya amani.
Ziara hiyo ya Berlin inajiri siku chache baada ya Urusi kufanya mojawapo ya mashambulizi yake mazito zaidiya makombora na ndege zisizo na rubani katika mzozo wa Ukraine, na huku Rais wa Marekani Donald Trump akieleza kusikitishwa kwake na Rais wa Urusi Vladimir Putin.