Zelensky: Urusi ivimalize vita ilivyovianzisha
18 Agosti 2025Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky amewasili mjini Washington kwa ajili ya mkutano wake na Rais wa Marekani Donald Trump, na amesema kuwa Urusi inapaswa kuvimaliza vita ilivyovianzisha.
Zelensky ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii waX kwamba wananchi wa Ukraine wanaipigania ardhi yao na uhuru wako. Aidha, amesema ana matumaini kwamba nguvu yao ya pamoja na Marekani, na marafiki wa Ulaya itailazimisha Urusi kushiriki katika amani ya kweli.
Zelensky amesema Urusi haipaswi ''kutuzwa'' kwa uvamizi wake. Ameyasema hayo, baada ya Trump kupendekeza kuwa Zelensky atalazimika kukubali kutorejeshewa Rasi ya Crimea, ambayo ilinyakuliwa na Urusi, mwaka 2014, na kwamba Ukraine haitoruhusiwa kujiunga na Jumuia ya Kujihami ya NATO, ili amani iweze kupatikana.
Mazungumzo hayo ambayo yatawashirikisha pia viongozi kadhaa wa Ulaya, yanafanyika siku chache baada ya Rais Trump kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin huko Alaska siku ya Ijumaa.
Kwa upande wake Rais Trump ametoa taswira ya mkutano huo ambapo amesema amepata 'heshima kubwa' kuwakaribisha viongozi wa Ulaya. Trump ameandika katika mtandao wake wa kijamii waTruth, kuwa leo ni siku kubwa katika Ikulu ya Marekani, White House, na ni heshima kubwa kwa Marekani. Trump anatarajiwa kukutana kwanza na Zelensky na kisha viongozi wa Uingereza, Ujerumani, Ufaransa, Italia, Finland, Umoja wa Ulaya na NATO.
Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye alihudhuria mkutano kati ya Trump na Zelensky mwezi Februari na kumalizika bila ya kuwepo maelewano, pia atahudhuria mazungumzo ya leo.
Keir Starmer: Ni lazima amani ya kudumu ipatikane Ukraine
Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer amesema washirika wa Ukraine lazima wahakikishe kwamba kuna amani ya haki na ya kudumu nchini Ukraine. Matamshi hayo ameyatoa leo wakati akisafiri kuelekea Washington kumuunga mkono Zelensky katika mazungumzo magumu na Rais Trump.
''Tunapaswa kuhakikisha kuna amani ya kudumu, ya haki, na ndiyo maana ninasafiri kwenda Washington na viongozi wengine wa Ulaya kulijadili hili ana kwa ana na Rais Trump na Rais Zelensky, kwa sababu ni kwa maslahi ya kila mtu, kwa maslahi ya Uingereza, kwamba tuipate haki hii,'' alisisitiza Starmer.
Starmer na viongozi wengine wa Ulaya wanatafuta kumshawishi Trump kutoshinikiza suluhu ambayo itampa Putin fursa ya kuhalalisha uchokozi wake, lakini pia inahakikisha usalama wa Marekani kwa kikosi chochote cha kijeshi cha kulinda amani kutoka katika kile kinachoitwa ''muungano wa hiari.''
Kulingana na kiongozi huyo wa Uingereza, vita vya Ukraine vimekuwa vikiendelea kwa muda mrefu sasa, miaka mitatu na zaidi, na vimewaathiri watu wa Ukraine ambao wameteseka sana, lakini pia vimeiathiri Ulaya.
Wakati huo huo, Balozi wa Ukraine nchini Ujerumani Oleksii Makeiev, amesisitiza uhitaji wa dharura katika kuhakikisha usalama kwa nchi yake. Akizungumza na kituo cha redio cha Ujerumani cha Deutschlandfunk kabla ya mkutano wa Trump na Zelensky mjini Washington badae Jumatatu, Makeiev amesema Kifungu cha 5 cha Mkataba wa NATO kiko wazi, kwa sababu kinawataka wanachama wa muungano huo wa kijeshi kuliona shambulizi dhidi ya mwanachama mmoja, kama shambulizi kwa wote.
(AFP, DPA, AP, Reuters)