Zelensky: Putin hana nia ya kusitisha mapigano
1 Septemba 2025Kauli hiyo amekuwa akiirudia mara kwa mara tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka 2022, na hivi karibuni Zelensky alithibitisha kuwa yuko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Putin ikiwa kutakuwepo mazingira ya kuaminika na dhamana za kimataifa zitakazohakikisha usalama wa Ukraine.
Katika hotuba yake ya jana jioni kupitia njia ya video, Zelensky ameeleza kwamba Marekani ilisema wiki mbili zilizopita kuwa Moscow ilipaswa kuwa tayari kufikia sasa kuandaa mkutano wa ngazi ya viongozi.
Masharti ya Ukraine yanabaki kuwa wazi: mazingira ya kuaminika, dhamana madhubuti za kimataifa na hakikisho la usalama wa taifa lake. Hata hivyo, kiongozi huyo amesema badala ya kuonyesha nia ya mazungumzo, "kitu pekee ambacho Urusi inachokifanya ni kuwekeza zaidi katika vita."
Akizungumzia kuhusu ziara ya Putin nchini China, Zelensky amemshtumu kwa mara nyingine kiongozi huyo wa Moscow kwa kujaribu kukwepa mazungumzo ya kuvimaliza vita hivyo akisema "huo ndio mchezo wake namba moja."
Nchi za Magharibi zaendelea kuiunga mkono Ukraine
Licha ya matarajio ya Marekani ya kuwepo mazungumzo ya moja kwa moja kati ya viongozi hao wawili – Putin na Zelensky, Urusi hadi sasa haijaonyesha utayari wa kushiriki mazungumzo hayo. Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov hivi karibuni aliweka bayana kwamba Putin amekataa kuzungumza na Zelensky, akitilia shaka uhalali wake kama rais wa Ukraine.
Zelensky anaendelea kuiongoza Ukraine chini ya sheria ya kijeshi, ambayo kwa mujibu wa katiba, inamruhusu kusalia madarakani hata baada ya muda wa kuhudumu kama rais kukamilika.
Kwa upande mwingine, Putin amebaki madarakani tangu mwaka 2012, akisaidiwa na marekebisho ya katiba yalioongeza ukomo wa mihula yake.
Wakati huo huo, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz ametahadharisha kuwa vita vya Ukraine vinaweza kuendelea kwa muda mrefu. Akizungumza katika mahojiano na shirika la habari la Ujerumani ZDF, kiongozi huyo amesema kwamba kuvikomesha vita hivyo haraka kwa hasara ya Ukraine sio chaguo lake.
Ameongeza kuwa ingawa hajakata tamaa kuhusu uwezekano wa usitishaji mapigano mwaka huu, "hana matumaini yasiyo na msingi."
"Namaanisha kuwa vita vinaweza kumalizika kesho—hata leo—ikiwa Ukraine itasalimu amri, iachane na mapambano na ipoteze uhuru wake. Lakini kesho yake, itakuwa zamu ya taifa jingine, na siku inayofuata, huenda ikawa zamu yetu. Hilo si chaguo langu."
Merz amesisitiza kwamba kipaumbele cha serikali ya Berlin ni kuendelea kuiunga mkono Ukraine katika kujitetea dhidi ya Urusi. Kansela huyo wa Ujerumani pia amepinga kupelekwa kwa wanajeshi wa ardhini nchini Ukraine kwa sasa.
Ameeleza kuwa, mjadala unajikita katika dhamana za kiusalama endapo mpango wa usitishaji mapigano utafikiwa.
Ujerumani imekuwa mfadhili mkuu wa Ukraine na imetoa au kuahidi msaada wa kijeshi wenye thamani ya euro bilioni 40 tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mnamo Februari 2022.