Zelensky na Vance kukutana mjini Munich
14 Februari 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy atakutana leo na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance mjini Munich kwa mazungumzo yanayotarajiwa kufungua pazia la mashauriano ya kumaliza vita kati ya Ukraine na Urusi.
Mazungumzo hayo yatakayofanyika kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kimataifa wa Usalama wa Munich baadaye hii leo, yatahudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Marco Rubio.
Soma pia: Zelensky kukutana na JD Vance mjini Munich siku ya Ijumaa
Yanafuatia tangazo la Rais Donald Trump wa Marekani la siku ya Jumatano kuwa mazungumzo ya amani na kumaliza vita vya Ukraine yataanza mara moja baada ya kiongozi huyo kuzungumza na Rais Zelensky pamoja na Vladimir Putin wa Urusi.
Mkutano kati ya Zelensky na Vance utagubikwa na kiwingu cha wasiwasi wa kiongozi huyo wa Ukraine na washirika wake wa Ulaya kwamba Marekani inaweza kufikia makubaliano na Urusi ya kumaliza vita bila kuishirikisha Ukraine. Zelensky alionya hapo jana kuwa atayapinga mazungumzo yoyote ya amani yatakayofanyika bila kuihusisha Ukraine.