Zelensky: Maelfu ya wanajeshi wanaweza kupelekwa Ukraine
5 Septemba 2025Dhamana hizo zinapendekezwa na washirika wa Ukraine, punde uvamizi wa Urusi nchini mwake ukimalizika.
Zelensky alisema hayo baada ya kukutana na Rais wa Baraza Kuu la Ulaya, Antonio Costa huko Uzhorod, magharibi mwa Ukraine. Alitilia msisitizo kuwa idadi ya wanajeshi hao itakuwa ni maelfu wala si mamia tu.
Kauli ya Zelensky ilikuwa sehemu ya jibu lake kwa mwandishi habari, huku akisema ni mapema sana kuzungumzia suala hilo kwa undani.
Mnamo Alhamisi rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema nchi 26 zimeahidi kutuma wanajeshi wake nchini Ukraine baada ya vita kumalizika, kama kikosi cha kimataifa kutoa hakikisho la usalama wa ardhini, majini na angani kwa taifa hilo dogo jirani ya Urusi.
Awali, Macron alisema nchi hizo zitatuma wanajeshi wao ndani ya Ukraine. Lakini baadaye alisema baadhi zitatoa dhamana za usalama bila ya kuingia katika ardhi ya Ukraine, kwa mfano kutoa mafunzo na vifaa vya vikosi vya Kiev.
Mapema Ijumaa, rais wa Urusi Vladimir Putin, alisema wanajeshi wowote wa kigeni watakaoingia Ukraine watakuwa walengwahalali wa kushambuliwa na vikosi vyake.
Huko Uzhhorod, Zelenskiy amesema "ameratibu hatua" za mazungumzo na Costa kuhusu Ukraine kujiunga na Umoja wa Ulaya. Kyiv inaona uanachama wa Umoja wa Ulaya kama ufunguo wa usalama na kupona kwake baada ya vita.
Zelensky pia likutana Ijumaa na Waziri Mkuu wa Slovakia Robert Fico. Kulingaa na naibu waziri wa nishati wa Ukraine Roman Andarak, Zelensky anatarajiwa kujadiliana na Fico kuhusu usafirishaji wa mafuta ya Urusi kupitia Ukraine.
Slovakia hutegemea pakubwa bidhaa za mafuta kutoka Urusi kupitia bomba la Druzhba ambalo miundo mbinu yake Ukraine ilishambulia hivyo kuvuruga usafirishaji, halia ambayo imeighadhabisha Slovakia.
Mnamo Jumanne, Fico alikutana na Rais Putinmjini Beijing China na akasema nchi yake inataka kuboresha uhusiano wa kawaida na Urusi.
Ukraine imezihimiza nchi nyingine kuacha kununua mafuta ya Urusi, ili kuinyima fedha inazotumia kufadhili vita vyake.
Siku ya Alhamisi, rais wa Marekani Donald Trump, aliwaambia viongozi wa Ulaya kwamba ni lazima wakome kununua mafuta ya Urusi. Hayo ni kwa mujibu wa afisa wa ikulu - White House.
Katika tukio jingine, Ukraine imesema imeshambulia kituo cha mafuta kilichoko jimbo la Ryazan nchini Urusi.
Mkuu wa vikosi vya droni vya Ukraine, Robert Brovdi, ameandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kuhusu mashambulizi ya kituo cha mafuta, umbali wa kilomita 200 kusini mashariki ya Moscow na kituo kingine katika jimbo la Luhansk linalodhibitiwa na Urusi.
Kama sehemu ya kampeni yake ya kujilinda, katika wiki za hivi karibuni, Ukraine imeimarisha mashambulizi yanayolenga miundombinu ya uzalishaji mafuta ya Urusi, ili kuhujumu operesheni za jeshi la nchi hiyo.
(DPAE,RTRE)