Zelensky azungumza baada ya majibizano makali na Trump
1 Machi 2025Zelensky ameyasema hayo alipohojiwa na kituo cha Fox News na kuongeza kuwa Ukraine inahitaji mno msaada wa Marekani ili kupambana na jeshi la Urusi alilolitaja kuwa na uwezo mkubwa wa wanajeshi na silaha bora zaidi.
Aidha, rais huyo wa Ukraine alisema wazi kuwa nchi yake haiwezi kuishinda Urusi bila ya msaada wa Marekani huku akionekana kujutia kilichotokea Ijumaa jioni:
" Nadhani halikuwa jambo zuri kwa sababu tulikuwa na tofauti nyingi kwenye mazungumzo hayo. Huwa kwa kawaida sifunguki sana kwenye vyombo vya habari lakini kuna mambo muhimu sana. Ninataka tu kuwa mkweli na kuhakikisha washirika wetu wanaelewa kwa usahihi hali halisi. Itakuwa vigumu kwetu bila msaada wao. Lakini hatuwezi kupoteza maadili yetu, watu wetu na hatuwezi kupoteza uhuru wetu. "
Soma pia: Mkutano wa Zelensky, Trump wamalizika vibaya
Hata hivyo Zelensky amekataa kuomba msamaha akisema hadhani kuwa alifanya kosa lolote. Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev alitumia kauli nzito dhidi ya Zelensky akimwita "nguruwe mkaidi" ambaye "ameadabishwa kwenye Ikulu ya White House". Chama cha Republican cha Trump kimeiunga mkono Urusi kwa kumlaumu Zelensky.