Zelensky atafuta maridhiano na Urusi na Trump
5 Machi 2025Zelensky, ambaye nchi yake imekuwa ikipambana na uvamizi kamili wa Urusi kwa miaka mitatu, pia ameweka wazi kuwa hana kinyongo kufuatia mkutano uliokumbwa na mkanganyiko na Rais wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita.
Amemshukuru Trump kwa uongozi wake na msaada wa silaha kwa Ukraine. Zelensky ameandika kwenye mtandao wa X kuwa Ukraine iko tayari kukaa kwenye meza ya mazungumzo haraka iwezekanavyo ili kuisogeza karibu amani ya kudumu.
Kiongozi huyo ameyasema hayo kufuatia tuhuma za Marekani kuwa hataki kumaliza vita hivyo, jambo lililosababisha Trump kusimamisha msaada wa kijeshi kwa Kiev.
Amesema hatua za kwanza huenda zikawa ni kuwaachia wafungwa na kusitisha mashambulizi ya kutokea angani - kupiga marufuku makombora, droni za masafa marefu, mashambulizi ya bomu kwenye miundombinu ya nishati na nyingine ya kiraia - na kusitisha mashambulizi ya baharini mara moja, ikiwa Urusi nayo itafanya hivyo." Zelensky amesema anatumai kuanzisha upya uhusiano na Washington na pia akasema bado yuko tayari kusaini mpango wa madini ili nayo Marekani iihakikishie Ukraine usalama.