Zelensky ahimiza misaada zaidi kwa ajili ya kuilinda Ukraine
10 Julai 2025Zelensky amesisitiza kwamba huo ndio msimamo unaohitajika sasa. Zelensky amesema haitakuwa sahihi kwa nchi washirika kuwa na uhaba wa fedha. Rais huyo wa Ukraine ameyasema hayo leo kwenye mkutano wa siku mbili unaofanyika mjini Rome kujadili ujenzi upya wa Ukraine.
Ameeleza kuwa Ukraine inahitaji silaha kwa ajili ya ulinzi wa anga yake na kwamba ni lazima kuyakomesha mashambulio ya droni na makombora yanayofanywa na Urusi. Rais Zelensky amewaambia viongozi kwenye mkutano huo kuwa mashamblio yanayofanywa na Urusi yanathibitisha kwamba Putin hataki amani.
Viongozi mbalimbali, miongoni mwao, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen na wakuu wa makampuni kadhaa wanahudhuria mkutano huo wa mjini Rome unaofanyika chini ya uenyekiti wa waziri mkuu wa Italia Giorgia Meloni.