Zelensky aelekea Saudia kutafuta mwafaka wa vita
10 Machi 2025Rais Zelensky anatazamiwa kukutana na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman ambaye nchi yake imekuwa na jukumu kubwa katika juhudi za upatanishi tangu uvamizi wa Urusi mwaka 2022, ikiwa ni pamoja na kuratibu mabadilishano ya wafungwa na kuwa mwenyeji wa mazungumzo baina ya Urusi na Marekani mwezi uliopita.
Mazungumzo ya Jumanne kati ya maafisa wa Marekani na Ukraine, yanatarajiwa kuangazia makubaliano ya nchi mbili ya madini na jinsi ya kumaliza vita. Mazungumzo hayo ni ya kwanza rasmi tangu kulipotokea sokomoko la majibizano makalikatika Ikulu ya White House kati ya Zelenskiy na Rais wa Marekani Donald Trump.
Soma zaidiUrusi na Ukraine zashambuliana vikali
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio alianza ziara ya Saudia jana Jumapili, wakati rais Trump akiamua iwapo atabadili dhamira yake ya kusitisha misaada ya kijeshi na kijasusi dhidi ya Ukraine. Katika mazungumo ya siku tatu mjini Jeddah, Rubio atajadili namna ya "kuendeleza dhamira ya rais ya kumaliza vita vya Urusi nchini Ukraine".
Mazungumzo ya Jeddah yatamshirkisha Rubio na mshauri wa usalama wa kitaifa wa Trump Mike Waltz, mshauri wa usalama wa Zelensky na mawaziri wa mambo ya nje na ulinzi. Marekani, ambayo zamani ilikuwa mshirika mkuu wa Ukraine, imebadili sera zake za kivita na sasa ikielekeza harakati zake katika kukomesha haraka mapigano, ikishirikiana moja kwa moja na Moscowhuku ikikata msaada wa kijeshi na kijasusi kwa Kyiv.
Soma ripoti hii: Marekani yasitisha kuipa Ukraine taarifa za intelijensia
Rais Donald Trump amenukuliwa katika mahojiano ya Jumapili na kituo cha Fox News akipendekeza kwamba Ukraine haiwezi kusalimika katika vita vyake na Urusi. Katika mahojiano hayo, Trump aliulizwa kama yuko sawa na ukweli kwamba amesimamisha misaada kwa Kyiv na akasema kwamba. "Kweli, haiwezi kusalimika lakini unajua, tuna udhaifu fulani na Urusi. Unajua inahusisha pande mbili na vita haikupaswa kutokea, na vimetokea. Kwa hivyo sasa tumekwama na suala hili."
Trump amemshutumu Zelensky kipindi cha nyuma kwa vita vilivyoanza wakati Urusi ilipoivamia Ukraine huku akimwongezea shutuma kiongozi huyo wa Ukraine kwamba hataki kuvimaliza vita.
Hayo yakijiri vikosi vya Urusi vimezidi kusonga mbele katika mkoa wa Kursk leo Jumatatu kama sehemu kubwa ya operesheni inayolenga kuwafurusha maelfu ya wanajeshi wa Ukraine katika eneo la magharibi mwa Urusi.
Soma: Urusi, Ukraine zaendelea kukabiliana vikali Kursk
Vikosi vya Ukraine vilikamata kiasi cha kilometa 1,300 za mkoa wa Urusi wa Kursk mnamo mwezi Agosti wakati Kyiv ikisema hiyo ilikuwa ni jaribio la kuchanga karata itakayoitumia katika majadiliano ya baadae na kuilazimisha Urusi kuondoa vikosi vyake mashariki mwa Ukraine. Lakini hadi kufikia katikati ya mwezi Februari Urusi ilikuwa imerejesha kilometa karibu 800 za eneo la Kursk.