Zelenskiy : Hakuna mpango wa mazungumzo ya amani bila sisi
15 Februari 2025Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema leo Jumamosi kwamba Ukraine kamwe haitokubali mpango wowote wa mazungumzo ya amani kati ya Urusi ambao hautoihusisha nchi yake moja kwa moja.
Zelenskiy ameyasema hayo katika mkutano wa kimataifa wa usalama unaofanyika mjini Munich akijibu tamko la Rais Trump wa Marekani aliyesema kwamba amezungumza na Rais Vladimir Putin wa Urusi juu ya mpango wa kuvimaliza vita hivyo vilivyodumu karibu miaka mitatu.
Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani asema nchi haitokubali watu wanaoingilia kati demokrasia ya Ujerumani
Rais huyo wa Ukraine ametoa mwito pia kwa Ulaya kuwa na jeshi lao na kwamba Ukraine pekee yake haiwezi kupigana vita kwa ajili ya usalama wao.
"Bila ya jeshi la Ukraine, majeshi ya Ulaya hayatatosha kuizuia Urusi , ndio uhalisia uliopo leo. Ni jeshi letu pekee barani Ulaya ambalo lina uzoefu halisi wa uwanja wa vita. Lakini jeshi letu pekee halitoshi. Na tunahitaji kile mnachoweza kutoa: silaha, mafunzo, vikwazo, ufadhili, shinikizo la kisiasa na umoja." amesema Zelenskiy.
Washirika wa Ukraine hasa barani Ulaya wameingiwa na wasiwasi tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipotangaza kwamba mazungumzo ya kumaliza vita vya Ukraine yataanza hivi karibuni baada ya kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Rais Vladimir Putin wa Urusi pamoja na Zelensky wa Ukraine.