Zelenskiy aelekea Paris kwa mazungumzo na Macron
26 Machi 2025Hii ni kabla ya mkutano wa kilele wa nchi zilizo tayari kusaidia kuhakikisha uwezekano wa makubaliano ya amani kati ya Ukraine na Urusi.
Ufaransa na Uingereza zimekuwa zikiongoza mpango wa kuunda kile kinachoitwa "muungano wa walio tayari," ambao utaundwa na nchi zilizojiandaa kutoa dhamana ya usalama iwapo mpango wa usitishaji mapigano kati ya Urusi na Ukraine utafikiwa. Wazo hilo litakamilishwa katika mkutano wa kilele Paris kesho Alhamisi.
Washirika wa Magharibi wa Ukraine wanafikiria kufuatilia uwezekano wa kuwa na eneo lisilo na kijeshi kwenye mpaka kati ya Urusi na Ukraine.
Wakati huo huo, Marekani imefikia makubaliano tofauti na Ukraine na Urusi, ambapo nchi hizo zimekubali kusitisha mashambulizi baharini na dhidi ya miundombinu ya nishati.
Hata hivyo, Urusi imesema makubaliano hayo kuhusu Bahari Nyeusi hayatatekelezwa hadi baadhi ya benki zake zirejeshwe katika mfumo wa kifedha wa kimataifa. Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesisitiza kuwa makubaliano hayo hayatakiwi kutegemea kuondolewa kwa vikwazo, akiiita kauli ya Ikulu ya Urusi, Kremlin jaribio la kujaribu "kuchezea" utekelezaji wa makubaliano hayo.