ZANZIBAR:Tutafuata nyayo za Ukraine kufanya mageuzi chama cha CUF chaarifu
17 Agosti 2005Chama kikuu cha upinzani visiwani Zanzibar nchini Tanazania CUF hapo jana kimetishia kufanya maandamano makubwa ya kuipinga serikali ya chama cha CCM visiwani humo kwa madai ya kupanga njama za kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi mkuu ujao.
Chama hicho kimearifu kwamba iwapo serikali haitochukua hatua yoyote juu ya madai yao basi kitafanya mageuzi sawa na ilivyofanyika nchini Ukraine mnamo mwaka jana.
Afisa wa chama cha CUF Ismail Jussa amesema chama hicho kimemtahadharisha kwa maandishi rais wa Tanzania anayeondoka madarakani Benjamin Mkapa pamoja na halmashauri ya uchaguzi visiwani Zanzibar kwamba kitatumia nguvu za wananchi kutetea haki yao.
Hatua ya chama hicho imefuatia Serikali kufutilia mbali tenda baina ya tume ya uchaguzi ya zanzibar na kampuni moja ya Afrika kusini iliyopewa jukumu la kuchunguza na kuthibitisha orodha ya wapiga kura waliojiandikisha kwa madai ya kutofuata maagizo ya tenda hiyo.
Hata hivyo halmashauri ya uchaguzi imesema italichunguza suala hilo.