ZANZIBAR : Polisi yajeruhi wafuasi 18 wa upinzani
10 Oktoba 2005Polisi ilitumia nguvu kutawanya umati wa wafuasi wa chama cha upinzani katika kisiwa chenye utete wa kisiasa cha Zanzibar nchini Tanzania hapo jana na kujeruhi watu 18 katika machafuko mapya kabla ya uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.
Mashahidi wamesema polisi wa kutuliza ghasia walitumia hewa ya kutowa machozi na magurunedi ya kushtuwa na kwa mujibu wa wengine wanasema risasi za moto zilitumika kutawanya mamia ya watu waliokuwa wakijaribu kwenda kwenye mkutano wa kampeni wa upinzani uliopigwa marufuku.
Imeelezwa kwa vikosi vya usalama vilifyetuwa mabomu 30 ya kutowa machozi na magurunedi ya mshutuko kwa umati wa watu katika mji wa Mahonda karibu na eneo la mkutano huo wa hadhara huko Donge kilomita 30 kaskazini mwa Mji Mkogwe wa Zanzibar.
Ingawa kumwekuwepo na habari za kutatanisha iwapo polisi walifyatua risasi za moto mashahidi kadhaa na duru za hospitali zinasema miongoni mwa watu hao 18 waliojeruhiwa watu walikuwa na majeraha ya risasi.
Msemaji wa chama cha CUF Salum Dimani amelaani kitendo hicho cha polisi wanaodaiwa kutumia risasi za moto kwa raia wasiokuwa na silaha na ametaka kujiuzulu kwa kamishna wa polisi wa visiwani.
Hivi mchana chama hicho cha CUF kimeitisha mkutano wa waandishi wa bahari mjini D’salaam kuzungumzia machafuko hayo.