Zaidi ya watu milioni 83 wakosa makaazi ndani ya nchi zao
13 Mei 2025Wakimbizi wapatao milioni 83.4 walisajiliwa mwaka jana 2024 – sawa na idadi jumla ya watu wanaoishi Ujerumani – kufuatia mizozo mikubwa katika ukanda wa Gaza na nchini Sudan, pamoja na mafuriko na vimbunga.
Kwa mujibu wa ripoti ya pamoja ya kila mwaka ya kituo cha ufuatiliaji wa wakimbizi wa ndani IDMC na baraza la Wakimbizi la Norway NRC, hiyo ni zaidi ya mara mbili ya idadi iliyorekodiwa miaka sita iliyopita.
Soma pia: UNHCR: Watu 800,000 waikimbia Kongo kutokana na mzozo
Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa karibu asilimia 90 ya wakimbizi wa ndani duniani kote, au watu milioni 73.5 walifurushwa kutoka makwao kutokana na mizozo na ghasia – ongezeko la asilimia 80 tangu mwaka 2018.
Takriban nchi 10 ziliripoti kuwa na zaidi ya wakimbizi wa ndani milioni tatu kila mmoja kufuatia mizozo na ghasia mwishoni mwa mwaka 2024, huku Sudan inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa na watu milioni 1.6 waliokimbia makaazi yao – idadi kubwa zaidi kuwahi kurekodiwa katika nchi moja, ripoti hiyo imeonyesha.