Maelfu ya Wasudan waendelea kuikimbia nchi
24 Juni 2025Wakati Jumuiya za Kimataifa na wasuluhishi wakiendeleza juhudi za kusaka amani, ripoti za vifo na ukiukwaji wa haki za binadamu zinaendelea kuongezeka kila uchwao.
Taarifa ya leo Jumanne za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinasema takriban watu 40 wameuawa baada ya shambulizi lililofanywa Jumamosi iliyopita katika Hospitali ya Al Mujlad, magharibi mwa Kordofan.
Miongoni mwa waliouawa ni watoto sita na wahudumu wa afya watano, huku hospitali hiyo ikiharibiwa vibaya. Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amelaani vikali mashambulizi yanayolenga vituo vya afya na kutaka wahusika kuwajibishwa haraka.
Sudan ilitumbukia kwenye mzozo tangu Aprili, 2023
Tangu Aprili 2023, Sudan imejikuta kwenye mgogoro mkubwa wa kiutawala kati ya mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan na kamanda wa RSF, Mohamed Hamdan Daglo.
Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, huku wengine zaidi ya milioni 13 wakiyahama makazi yao wakiwemo milioni nne waliokimbilia nje ya nchi.
Umoja wa Mataifa umetaja mgogoro huu kuwa janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani kwa sasa.
Ujumbe Huru wa Kimataifa wa Kutafuta Ukweli umesema kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya silaha nzito katika maeneo yenye wakazi wengi, sambamba na kuongezeka kwa kasi kwa ukatili wa kingono na madhila mengine ya kibinadamu.
Joy Ngozi Ezeilo, mtaalamu wa ujumbe huo wa uchunguzi wa kimataifa kuhusu mzozo wa Sudan, amesema hali ya mateso kwa raia, hususan wanawake na walioko mahabusu, imefikia viwango vya kutisha.
"Wasudan wengi wanakufa kwa njaa, na hasa wale waliokamatwa na walioko mahabusu... wanakufa. Na idadi ya walioathirika na njaa kali kabisa inaendelea kuongezeka kila siku,” alisema Ezeilo.
Uingizwaji wa silaha Sudan wachochea mzozo
Wachunguzi huru wa haki za binadamu nchini Sudan wamesema mapigano makali yanayoongezeka kila uchao ni matokeo ya moja kwa moja ya uingizwaji wa silaha unaoendelea nchini humo, licha ya kila upande unaotuhumiwa kuhusika na msaada wa kijeshi kwa kundi la RSF umekana kuhusika.
Umoja wa Mataifa umezishutumu pande zote mbili za mzozo, jeshi na RSF kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huku ukielezea wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kwa mashambulizi ya kikabila, hasa katika maeneo ya Darfur na Kordofan.
Ripoti zinaeleza kuwa wapiganaji wa RSF na wanamgambo wa Kiarabu wanaendeleza mashambulizi dhidi ya jamii za Zaghawa, Masalit na Fur, hali inayochochea hofu ya mauaji ya halaiki.
Mwezi uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Sudan dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu madai ya kushiriki katika mauaji ya halaiki kwa kuiunga mkono RSF, kwa maelezo kuwa haina mamlaka ya kisheria kuisikiliza.