Zaidi ya raia 21 wauwawa na ADF Mashariki mwa DRC
27 Julai 2025Watu wasiopungua 21 wameuawa siku ya Jumapili, kufuatia shambulio lililofanywa na waasi wanaoungwa mkono na kundi la itikadi kali linalojiita dola la Kiislamu, IS, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Soma pia: Kongo, M23 wasaini makubaliano ya kusitisha vita
Kwa mujibu wa Dieudonne Duranthabo,ambaye ni mratibu wa shirika la kiraia katika eneo la Komanda, aliyezungumza na shirika la habari la AP, waasi wa ADF mnamo majira ya saa saba usiku walivamia na kushambulia majengo ya kanisa katoliki kwenye eneo la Komanda mashariki mwa Kongo, kuteketeza majumba kadhaa na maduka.
Zaidi ya watu 21 wameuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa ndani na nje ya Kanisa hilo, amesema Dieudonne Duranthabo,na miili isiyopunguwa mitatu imeondolewa huku mingine ikitafutwa wakati msemaji wa jeshi la Kongo katika mkoa wa Ituri ambako kinapatikana kijiji cha Komanda amethibitisha kwamba watu 10 wamekufa.
Luteni Jules Ngongo amesema taarifa walizonazo mpaka kufikia asubuhi ya Jumapili, zinasema waasi waliojihami kwa mapanga walivamia kanisa karibu na Komanda na watu 10 wameuwawa na maduka kadhaa yakateketezwa kwa moto .
Baadhi ya raia wameanza kukikimbia kijiji hicho wakielekea mjini Bunia huku mwito ukitolewa kwa jeshi la Kongo kuingilia kati haraka kuwasaidia raia.Soma pia: Mvutano mpya watikisa juhudi za amani mashariki mwa DRC
Kundi la waasi la ADF liliundwa na wanachama wa makundi madogo madogo ya wapiganaji nchini Uganda katika miaka ya mwisho mwa 1990 kufuatia madai ya kutoridhishwa na utawala wa rais Yoweri Museveni.
Mnamo mwaka 2002 kufuatia kuandamwa na jeshi la Uganda waasi hao wakahamishia shughuli zao katika jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na tangu wakati huo, limehusika na hujuma za mauaji ya maelfu ya raia.
Mwaka 2019 lilijitangaza kuliunga mkono kundi la itikadi kali linalojiita dola la kiislamu.