Zaidi ya watu 200 waangamia kwa mafuriko Pakistan na India
15 Agosti 2025Zaidi ya watu 200 wamekufa kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa katika mkoa wa Kashmir huko India na nchi jirani Pakistan.
Kuna hofu kuwa idadi hiyo itaendelea kuongezeka kwa sababu idadi isiyojulikana ya watu bado hawajulikani waliko.
Maafisa wamesema jumla ya watu 164 wameripotiwa kufa katika eneo la Himalaya nchini Pakistan katika zaidi ya saa 24 zilizopita, huku mamia ya wafanyakazi wa uokozi na askari wakipelekwa kuwatafuta manusura wanaoaminika kusombwa na maporomoko ya ardhi na maji ya mafuriko.
Juhudi za uokozi zinatatizwa na mvua inayoendelea kunyesha na hofu ya kutokea mafuriko zaidi. Maafisa wamesema kiasi ya watu 167 wameokolewa katika eneo laKishtwar,wakiwemo 38 waliokuwa na majeraha mabaya.
Maafisa wa jeshi na wa Kitengo cha Kusimamia Majanga, wakisaidiwa na matrekta, wanaendelea kuondoa miamba, miti iliyong'oka na nguzo za umeme zilizoanguka ili kuwatafuta manusura na waliokufa.