Miili ya waliouawa yashuhudiwa Sweida, utulivu warejea
21 Julai 2025Katika mitaa ya mji wa Sweida, kando ya kutapakaa kwa miili ya watu waliouawa, moto uliripotiwa kuonekana katika maeneo mbalimbali ya mji huo jana Jumapili. Ni baada ya zaidi ya wiki moja ya mzozo kati ya wanamgambo wa Druze na makundi ya wapiganaji wa jamii ya Bedui.
Makubaliano tete ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Marekani na kutangazwa Jumamosi yalianza kutekelezwa Jumapili. Hatua hiyo sasa imeyasimamisha machafuko hayo yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100 ndani ya wiki moja.
Familia za jamii ya Bedui zaondolewa Sweida
Kutokana na machafuko hayo, mamlaka za Syria kwa kushirikiana na shirika la hilali nyekundu lmapema Jumatatu zimesema zimezihamisha familia za jamii ya Bedoui kutoka katika mji huo. Kulingana na Shirika la Habari la Syria SANA, miongoni mwa watu 1,500 waliohamishwa wakiwemo wanawake na watoto wamepelekwa katika eneo jirani la Daraa na kwenye mji mkuu Damascus.
Mapigano kati ya wanamgambo wa madhehebu ya Druze ambayo ni jamii ya walio wachache dhidi ya makabila ya Bedui ambayo wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni yametishia kuiteteresha Syria ambayo bado iko katika kipindi cha mpito baada ya vita.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM, zaidi ya watu 128,00 wamelazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na machafuko hayo yaliyoanza kwa vitendo vya utekaji na mashambulizi wiki moja iliyopita.
Zaidi ya hapo, Israel pia iliifanya mashambulizi kadhaa ya droni katika mji wa Sweida ikivilenga vikosi vya serikali ambavyo vilikuwa upande wa makabila ya Bedui. Pia, baadhi ya mashuhuda na moja ya mashirika yanayofuatilia hali mjini humo yamevishutumu vikosi vya serikali ya Syria kwa kufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji holela mara tu vilipoingia Sweida wiki iliyopita.