Zaidi ya watu 100 wauawa mafuriko ya usiku mashariki mwa DRC
12 Mei 2025Tukio hilo lilisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa muda mrefu, ikisindikizwa na upepo mkali, na kusababisha maporomoko ya ardhi yaliyozikwa baadhi ya nyumba.
Kwa mujibu wa Mkuu wa wilaya ya Fizi, Sammy Kalonji, tukio hilo limeacha majonzi makubwa huku mamia ya familia zikipoteza makazi na mali zao. Maeneo matatu ya kijiji hicho yameripotiwa kufukiwa kabisa na tope, na juhudi za kuwaokoa waliokwama au kupata miili ya waliopotea zinaendelea.
Kazi ya uokoaji inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya wakaazi wa eneo hilo na maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu, huku baadhi ya watu wakitafuta miili ya wapendwa wao kandokando ya ziwa Tanganyika kwa hofu kuwa huenda waathirika waliosombwa na maji waliishia ziwani.
Soma pia: Watu wa 8 wamekufa kwa ajali ya moto.
Dominike Asakya, msimamizi wa Shirika jipya la raia wilayani Fizi, amesema juhudi hizo zinakumbwa na vikwazo vikubwa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya kisasa na usaidizi wa haraka wa dharura.
"Changamoto kubwa ni miundombinu duni, ukosefu wa barabara na vifaa vya uokoaji. Hali ni mbaya, lakini watu wanajitahidi kwa kila hali,” amesema Asakya.
Maafa haya yamezuka wakati wilaya ya Fizi ikiwa chini ya tahadhari kubwa kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya vikosi vya serikali ya Kongo na washirika wake wa ndani na kutoka Burundi dhidi ya makundi ya waasi wa Twirwaneho na AFC/M23, yanayodaiwa kupata msaada kutoka kwa jeshi la Rwanda.
Soma pia: DRC yaandaa maombolezo ya kitaifa kwa waliouawa na mafuriko
Katika wito wa dharura, Jacques Alimasi, msimamizi wa mashirika ya kiraia wilayani Fizi, amezitaka pande zote katika mgogoro kuruhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko hayo.
"Tunaziomba pande zote kuweka silaha chini kwa muda na kuruhusu mashirika ya misaada kuingia. Maisha ya watu yako hatarini,” amesema.
Siku moja baada ya maafa hayo, mafuriko mengine yameripotiwa katika kijiji cha Bubale yapili, wilayani Kalehe, ambapo zaidi ya nyumba 50 na shule zimeharibiwa kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na maji ya mteremko.