Zaidi ya Wapalestina 50,000 wameuawa katika vita vya Gaza
24 Machi 2025Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti kuwa idadi ya Wapalestina waliouawa kwenye vita vinavyoendelea imepita watu elfu 50, ingawa takwimu hizi haziwezi kuthibitishwa kwa njia huru, lakini mashirika ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa yanazichukulia kuwa za kuaminika kwa kiasi kikubwa.
Vita hivyo vilianza baada ya kundi la Hamas kushambulia Israeli Oktoba 7, 2023, ambapo takriban watu 1,200 waliuawa na zaidi ya 250 kuchukuliwa mateka. Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki sita, mashambulizi ya Israeli yameendelea wiki hii na kusababisha vifo vya mamia zaidi ya Wapalestina.
Soma pia: Hamas yapinga wazo la Trump la kuwahamisha Wapalestina Gaza
Katika mashambulizi mapya, watu wapatao 30 wameuawa kusini mwa Gaza, wakiwemo viongozi wawili wa juu wa Hamas, Ismail Barhum na Salah al-Bardawil. Jeshi la Israeli limesema mashambulizi yake yamewalenga viongozi wa Hamas wanaotumia maeneo ya raia, ikiwemo hospitali, kama ngao, na lilikuwa limewataka wakazi kuondoka kwenye maeneo ya mapigano.