Yalizochambuliwa na wahariri wa Ujerumani hii leo
1 Juni 2006Kupungua mno idadi ya wasiokua na ajira nchini Ujerumani ndio mada iliyohanikiza ndani ya magazetini ya humu nchini hii leo.Mada ya pili ni kuhusu kuuliwa raia wa Irak na wanajeshi wa Marekani.
Idadi ya wasiokua na kazi imepungua kwa zaidi ya watu laki mbili na nusu na kusalia watu milioni nne na laki tano na 45 elfu.Upungufu wa watu laki tatu na nusu ikilinganishwa na mwaka jana.Serikali kuu ya ujerumani inaamini mageuzi yanaanza kuleta tija.Kuhusu mada hiyo gazeti linalochapishwa mjini Düsseldorf WESTDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:
“Laki mbili na nusu kamili wamepungua mwezi uliopita katika orodha ya wasiokua na ajira-ni habari nzuri hizo na za kutia moyo.Kiwango kama hicho hakijawahi kushuhudiwa katika kipindi cha mwezi mmoja,tangu muungano,shughuli za kiuchumi zilipokua zikinawiri.
Habari hizo nzuri hazimfanyi mtu asahau hata hivyo kwamba nchini Ujerumani bado kuna watu zaidi ya milioni nne na laki tano wasiokua na ajira.Na zaidi ya hayo kuna shaka shaka,takwimu hizo zimekujaje.”
Gazeti la DIE WELT la mjini Berlin linaonya:
„Bado ni mapema mno kuzungumzia juu ya mkondo wa mageuzi katika soko la ajira.Takwimu hizo za kuvutia ni matokeo tu ya msimu wa machipuko.Pirika pirika za kombe lijalo la dunia nazo pia zimechangia pengine katika hali hiyo.Cha kustaajabisha lakini ni kwamba walala hoi wa muda mrefu hawajafaidika hata kidogo na neema ya msimu wa machipuko.
Katika wakati ambapo wale wasiokua na ajira- ambao wamekua wakisaidiwa tangu mwaka mmoja au chini ya hapo,idadi yao imepungua sana,wakosa ajira wa muda mrefu zaidi,idadi yao haijapungua.Ni onyo hilo kwa washirika katika serikali ya muungano,wasije wakajibwaga vitini ,waakitaraji ukuaji wa kiuchumi utarekebisha yaliyosalia.Mapambano halisi dhidi ya ukosefu ajira bado hayajaanza.“
Gazeti la MAINZER ALLGEMEINEN ZEITUNG lina maoni sawa na hayso.Linaandika:
„Zaidi ya watu laki mbili na nusu wameajiriwa upya mwezi uliopita wa May-bila ya shaka ni jambo la kufurahisha hilo kwa wahusika.Lakini mtu akichunguza kwa makini,hatokosa kugundua,takwimu hizo zilizotangazwa mjini Nürnberg zinamaanisha kitu kimoja tuu nacho ni kwamba msimu wa baridi umemalizika.
Na jengine lililobainika takwimu zilipotangazwa jana ni kwamba,tukilinganishwa na takwimu za mwaka mzima,basi waliopungua katika orodha ya wasiokua na ajira ni watu 88 elfu tuu.Kwa maneno mengine yaliyoshuhudiwa katika soko la ajira katika enzi za neema,miongo iliyopita,yako mbali kufikiwa,seuze tena bado ajira nchini Ujerumani inawekewa vipengee vya kila aina na vyenginevo ni ghali kupita kwengineko.“
Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linahisi,mageuzi zaidi yanahitajika ili kuhakikisha matunda ya ukuaji wa kiuchumi yanaenea pia katika soko la ajira.
Mada ya pili magazetini inahusu kuuliwa raia 24 wa Irak na wanajeshi wa Marekani mjini Haditha.
Gazeti la NEUE OSNABRÜCKER linaandika
„Ikidhibitika kwamba wanajeshi wa nchi kavu wa Marekani wameuwa watu makusudi na mpata mpatae huko Haditha,litakua jambo la kushtuwa kupita kiasi.Itamaanisha wanajeshi wamejiamulia kulipiza kisasi ,wakenda kinyume na jukumu lao na kanuni za vikosi vya Marekani.Madhara yake hayatakua na kifani kwa Marekani yebnyewe na kwa usalama wa wanajeshi wake nchini Irak.