YALIYONDIKWA LEO NA MAGAZETI YA UJERUMANI
2 Desemba 2003Hii leo mada kuu za wahariri katika Magazeti ya Kijerumani zinahusika na hutuba ya kiongozi wa Chama cha Upinzani, CDU Bibi Angela Merkel mwanzoni mwa mkutano mkuu wa chama mjini leipzig. Mada nyingine zilihusika na hali nchini Iraq na ziara ya Kansela Gerhard Schröder nchini Uchina:
Kuhusu hutuba ya kiongozi wa chama cha CDU Bibi Angela Merkel, gazeti la DIE WELT linaandika: "Ilikuwa makini hutuba ya Bibi Merkel. Mjini Leipzig chama cha CDU kimenyanyua haiba yake kama chama cha maendeleo mapya. Hata hivyo, sifa hiyo inaweza kuwa pia kizingiti kwa chama kinachohitaji kuwahakikishia wapiga kura kuwa ndicho chama pekee chenye uwezo wa kurekibisha hali zao kulinganishwa na siasa ya marekibisho inayohitaji kufuatwa na vyama tawala. Lakini upande wao, wapiga kura wamekwisha ngamua kuwa marekibisho ya ubovu wa sasa hayawezi kuleta mabadiliko yoyote na kwamba kinachohitajika sasa ni fikara mpya."
Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU linaandika: "Miaka mitatu kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, hutuba ya kiongozi wa CDU isifahamike kama programu mpya ya ile inayoweza kuwa serikali yake, bali zaidi kama tangazo la maazimio. Kwa maneno mengine Bibi Angela Merkel amekipa chama chake mafunzo ya makini juu ya hila za kuendesha serikali. Na mkutano mkuu wa chama mjini Leipzig umeonyesha kuwa chama cha CDU kimekwisha jiandaa kujifunza somo la kuendesha serikali. Ni swali jengine iwapo kweli chama kinayajua kweli matatizo yanayokikabili, japokuwa kiongozi wake ameahidi kupambana nayo."
Upande wake, gazeti la RHEINPFALZ linaandika: "Katika siasa ya afya, malipo ya ustaafu, ajira ya kazi na kodi, Bibi Merkel amekiongoza chama cha CDU katika njia ya marekibisho ambayo itakuwa sahihi kwa Ujerumani. Kiongozi wa chama cha CDU amezikamata vyema hatamu za uongozi na kuwa mwanasiasa wa mbele kabisa katika chama hicho cha upinzani. Ameonyesha kuwa ana shabaha ya kukiteka kiti cha Kansela kwa kutoa programu madhubuti ya serikali."
Likiandika juu ya mada nyingine, gazeti la NÜRNBERGER ZEITUNG linaichambua hali nchini Iraq baada ya kutokea mapigano makali mjini Samarra: Gazeti hilo linaendelea kuandika: "Japokuwa hapo awali iliibuka fikra kuwa hakuna mpangilio maalumu katika yale mapigano ya upinzani nchini Iraq. Lakini sasa baada ya kutokea mapigano ya umwagaji damu katika mji wa Samarra tunapaswa kuamini kuwa mapigano hayo ya upinzani yamepangiliwa muda mrefu na uongozi wa zamani wa Iraq. Hivi sasa ziko ishara kwamba, kwa kuwa mtawala wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alijua kuwa hana nguvu za kijeshi za kupambana na wanajeshi wa Kimarekani, alivinadaa vikosi vyake kupigana aina ya vita vya kigaidi dhidi ya wavamizi." Na hatimaye gazeti la HEILBRONNER STIMME likigusia juu ya ziara ya Uchina ya Kansela Gerhard Schröder linaandika: "Mada ya haki za binadamu haina budi kuambatanishwa na ziara ya Uchina ya viongozi wa Kijerumani. Kwa sababu hiyo inasikitisha kuwa Kansela Schröder hakwenda Uchina kuishinikiza serikali ya Beijing bali kinyume cha mambo, amekwenda na risala ya niya njema ya kumalizwa vikwazo vya silaha dhidi ya Uchina. Upande wake, kiuchumi Uchina ni miongoni mwa madola yenye nguvu duniani, ndiyo maana haihitaji kupewa funzo la haki za binadamu na Ujerumani. Kinyume cha mambo, Kansela Schröder anaiotumia ziara yake kuitafutia Ujerumani tija za kibiashara nchini Uchina."